Feb 05, 2024 07:27 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Februari 5

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Kombe la Asia; Iran yaicharaza Japan na kutinga nusufainali

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumamosi ilishuka dimbani kuvaana na Japan katika mchuano wa aina yake wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Asia nchini Qatar, na kuambulia ushindi wa mabao 2-1, japo kwa mbinde. Mkwaju wa penalti wa dakika za mwisho wa Alireza Jahanbakhsh uliipa Iran ushindi huo dhidi ya wanasamurai wa Japan na kuiwezesha timu hii ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu kutinga nusu fainali ya Kombe la Asia kwa mara ya pili tangu 2004. Jahanbakhsh alitulia wakati wa mkwaju wa penalti katika dakika ya 96 na kuifanya Iran ambayo ilikosa huduma za mshambuliaji nyota Mehdi Taremi isonge mbele huku ikiwa na matumaini ya kutwaa taji hilo mwaka huu.

'Team Melli' ya Iran

 

Iran ilirejea katika mechi baada ya Hidemasa Morita kuifungia Japan, katika kipindi cha kwanza cha mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Education City nchini Qatar. Japan awali ilikuwa imetajwa kama timu ambayo ilikuwa na nafasi kubwa ya kunyakua Kombe la Asia mwaka huu. Mohammad Mohebi alisawazisha bao hilo dakika ya 55. Iran sasa itamenyana na Qatar katika ngoma ya nusu fainali siku ya Jumatano. Mwenyeji huyo Jumamosi usiku aliichachafya Uzbekistan mabao 3-2 katika mechi myingine ya robo fanali, baada ya kumaliza dakika 90 za ada na nyongeza kwa sare ya bao 1-1. Nusu fainali nyingine itazikutanisha Korea Kusini na Jordan. Iran ilitinga robo fainali baada ya kuitandika Syria mabao 5-3 katika upigaji matuta, baada ya dakika za ada na nyongeza kumaliza kwa sare ya bao 1-1. Vijana hao wa Kiirani wanaonolewa na Amir Ghalenoei wanapania kuhitimisha ukame wa miaka 47 wa kutwaa taji hilo la kieneo. Korea Kusini ilitangulia nusu fainali baada ya kuisasambua Australia mabao 2-1.

Karate; Iran yachota medali

Wanamichezo wa Iran wamemaliza mashindano ya Ligi Kuu ya Karate 1 kwa kuzoa medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba.  Mashindano hayo ya kimataifa ya siku 3, ambayo ndio muhimu na makubwa zaidi katika ulimwengu wa karate yalifunga pazia lake Jumapili huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Dhahabu ya Iran kwenye mashindano hayo ya dunia ilitwaliwa na Atousa Golshadnejad katika safu ya makarateka wa kike wenye kilo 61.

 

Karateka mwingine wa Kiirani, Mobina Heydari, aliipa Iran medali ya fedha katika kategoria ya wenye kilo 68, huku Ali Meskini akiishindia nchi hii medali ya shaba katika safu ya wanakarate wa kiume wenye kilo 60.

Robofainali za AFCON

Nigeria ambao ni mabingwa mara tatu wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) walikuwa wa kwanza kufuzu kwa hatua ya nusu-fainali ya mashindano hayo ya kibara ya mwaka huu nchini Ivory Coast, baada ya kuitandika Angola bao 1-0 katika Uwanja wa Felix Houphouet Boigny jijini Abidjan mnamo Ijumaa. Bao la pekee katika pambano hilo la robo fainali lilipachikwa wavuni na fowadi Ademola Lookman anayepiga soka la kulipwa katika ligi ya Serie A ya Italia. Lookman, 26, sasa ana mabao matatu kapuni na ni miongoni mwa masogora wanaopigiwa upatu wa kuibuka wafungaji bora kwenye duru hii ya 34 ya AFCON.

Wakati huohuo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilitoka nyuma na kuishinda Guinea kwa mabao 3-1 katika uwanja wa De La Paix mjini Bouake. Batoto ba Kongo walijicheza kufa kupona kwenye mchezo huo wa robo fainali. Mohamed Bayo aliwaweka Guinea kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 20 iliyosababishwa na Chancel Mbemba. Hata hivyo, Mbemba huyo alisawazisha mambo dakika saba baadaye kabla ya DRC kufunga magoli mengine kupitia penalti ya Yoane Wissa na ikabu ya Arthur Masuaku. Wanalingala hao sasa wametinga nusu-fainali itakayopigwa Februari 7 jijini Bouake.

Afrika Kusini Jumamosi usiku iliambulia ushindi wa mabao 2-1 katika upigaji matuta ilipochuana na Cape Verde katika mchezo mwingine wa robofainali baada ya kutoshana nguvu katika dakika za ada. Sasa Bafana Bafana watachuana na Super Eagles kwenye nusu fainali itakayopigwa Jumatano ijayo, huku DR Kongo ikitazamiwa kutoa jasho na wenyeji Ivory Coast. Hii ni mara ya kwanza kwa DRC kufuzu kwa nusu-fainali ya AFCON tangu mwaka wa 2015, ambapo wenyeji Equatorial Guinea waliwafunga mabao 4-2 kwenye upigaji penati, kufuatia sare tasa kwenye pambano la kutafuta mshindi nambari tatu. Wenyeji hao wamesogea mbele baada ya kuicharaza Mali mabao 2-1 katika mchezo mwingine wa robofainali ya kufa kupona siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Bouake. Mabao ya Kodivaa yalifungwa na Simon Adingra kunako dakika ya 90, huku Oumar Diakite alilizamisha jahazi la Wamali kwa goli lake la dakika za majeruhu katika muda wa nyongeza.

Dondoo za Hapa na Pale

Shirikisho la Soka Asia Magharibi (WAFF) limetoa mwito wa kusimamishwa utawala wa Israel kushiriki mashindano na shughuli zote zinazohusiana na kandanda duniani, kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na Tel Aviv katika Ukanda wa Gaza. Mwito huo ulitolewa Alkhamisi na Rais wa shirikisho hilo, Mwanamfalme Ali bin Hussein katika barua yake ya wazi kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, mashirikisho na vyama vya soka duniani pamoja na wanachama wake. Sehemu ya barua hiyo inasema: Unganeni nasi kuchukua msimamo madhubuti dhiti ya dhulma zinazofanyika Palestina na jinai za kivita zinazoendelea Gaza.

Rais wa shirikisho la WAFF, Mwanamfalme Ali bin Hussein

 

Mbali na kutaka kutengwa Shirikisho la Soka la Israel na kutoruhusiwa kushiriki katika shughuli zozote za soka madhali Tel Aviv inaendeleza mauaji ya kimbari Gaza, Rais wa WAFF ametaka wahusika wote waliotumiwa barua hiyo wakiwemo makocha, marefa, wachezaji na maafisa wa mashirikisho ya soka duniani kwa kauli moja walaani mauaji ya raia wasio na hatia Gaza na uharibifu wa miundimbinu ya soka katika eneo hilo.  

Katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Arsenal iliambulia ushindi wa kishindo Jumapili usiku nyumbani Emirates ilipovaana na Liverpool iliyotuama kileleni mwa EPL. Gunners waliichabanga Liverpool mabao 3-1 katika mchezo huo wa kuhemeshana, na hivyo kupunguza mwanya wa tofauti ya alama kati yake na Liverpool mbali na kukwea hadi katika nafasi ya pili kwenye msimamo ligi hiyo. Mabao ya Wabeba Bunduki katika mchezo huo yalifungwa kinda Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Leandro Trossard, huku la kufutia machozi la Liverpool likiwa la kujifunga la Gabriel Magalhaes. Arsenal sasa wamefikisha alama 49, alama mbili nyuma ya Liverpool, huku Manchester City wakifunga orodha ya tatu bora kwa alama 46. Mashetani Wekundu wikendi pia walivuna ushindi mnono wa mabao 3-0 walipochuana na West Ham nyumbani Old Trafford na kufikisha pointi 38, huku wakiridhika kutulia katika nafasi ya 6 kwa sasa kwenye jedwali la EPL. Mabao ya Man United kwenye mechi hiyo yalifungwa na Rasmus Hojlund, huku Alejandro Ganacho akicheza na nyavu mara mbili.

Mbali na hayo, serikali ya Tanzania imesema inatarajia kuanzisha somo la uchambuzi wa habari za michezo katika vyuo vinavyofundisha masomo ya uandishi wa habari kama ambavyo tayari imekwishaanza mchakato wa kuhakikisha chuo cha michezo cha Malya kinakuwa na mtaala wa kufundisha uchambuzi wa michezo kwa ajili ya kuongeza mtaala wa uchambuzi wa habari za michezo. Hayo yameelezwa Ijumaa hii ya Februari 2 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo Lushoto, Rashidi Shangazi aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuendeleza wachambuzi wa soka ili wawe na utaalamu wa kutosha katika kazi hiyo.

Na timu ya taifa ya wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 ya Kenya almaarufu Junior Starlets, imefuzu raundi ya tatu ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2024, baada ya wapinzani wao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiondoa mashindanoni. Kenya ilitarajiwa kwenda Kinshasa kucheza mechi hiyo ya kwanza ya mkondo wa pili Jumapili, lakini haikusafiri. Mechi ya marudiano ilikuwa imepangwa kuchezwa mnamo Februari 9, jijini Nairobi.

 

……………….TAMATI…………..

 

Tags