Brazil yamuita nyumbani balozi wake wa Israel, mzozo watokota
https://parstoday.ir/sw/news/world-i108608-brazil_yamuita_nyumbani_balozi_wake_wa_israel_mzozo_watokota
Serikali ya Brazil imemrejesha nyumbani balozi wake wa Israel, huku mzozo wa kidiplomasia ukiendelea kutokota baina ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini na Tel Aviv.
(last modified 2024-02-20T12:52:41+00:00 )
Feb 20, 2024 12:52 UTC
  • Brazil yamuita nyumbani balozi wake wa Israel, mzozo watokota

Serikali ya Brazil imemrejesha nyumbani balozi wake wa Israel, huku mzozo wa kidiplomasia ukiendelea kutokota baina ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini na Tel Aviv.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil imesema nchi hiyo imemrejesha nyumbani balozi wake wa Israel, Mauro Vieira  kwa ajili ya 'mashauriano' sanjari na kumuita balozi wa Tel Aviv mjini Brasilia, Daniel Zonshine kulalamikia kauli iliyotolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel.

Waziri huyo mwenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni, Israel Katz, siku ya Jumapili alitoa maneno makali dhidi ya Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil kwamba: "Hatutasahau na hatutasamehe. Ni shambulio hatari dhidi ya 'Wayahudi. Maneno ya Rais wa Brazil ni ya aibu na hatari, na hakuna mtu atakayedhuru haki ya Israeli ya kujihami."

Tel Aviv jana Jumatatu ilisema kuwa Rais wa Brazil atasalia kuwa si mtu anayekaribishwa kuitembelea Israel mpaka abadilishe kauli zake zinazovifananisha vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya "Holocaust" yanayodaiwa kufanywa na Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Waislamu wa Brazil katika maandamano

Rais Luiz Inacia Lula da Silva wa Brazil ameendelea kulaani vikali vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, utawala huo unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Viongozi wa Brazil wanasisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa na taasisi zake kama Baraza la Usalama lazima ziwe na ujasiri wa kuhakikisha kuwa inaundwa nchi huru ya Palestina.