Feb 25, 2024 02:35 UTC
  • Wataalamu wa UN: Kuipelekea silaha Israel kukomeshwe mara moja!

Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limeonya kwamba upelekaji wowote wa silaha au risasi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zitatumika katika mashambulizi ya ardhini na angani dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghazza uliozingirwa unaweza ukawa unakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, na lazima ukomeshwe mara moja.

Wataalamu hao wa UN wameeleza katika taarifa yao ya pamoja kwamba, mataifa yote lazima yahakikishe sheria ya kimataifa ya kibinadamu kwa wahusika kwenye mzozo wa silaha inaheshimiwa, kama inavyotakiwa na Mikataba ya Geneva ya 1949 na sheria zinazokubalika kimataifa.
 
Taarifa ya wataalamu hao imebainisha kuwa, ni lazima nchi zijiepushe kupeleka silaha yoyote au risasi kwa pande zinazozozana, ikiwa inatarajiwa, kutokana na hali halisi au mwenendo ulioonyeshwa huko nyuma kwamba, silaha hizo zitatumika kukiuka sheria za kimataifa.
 
Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameongeza kuwa upelekaji silaha ungali unapigwa marufuku hata kama serikali inayosafirisha silaha hizo nje haina nia ya kutaka silaha zitumike kinyume na sheria, au haijui kwa uhakika kwamba zitatumiwa kwa njia hiyo.

Taarifa ya wataalamu hao imepongeza pia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa ya Uholanzi mnamo Februari 12, ilipoiamuru serikali ya nchi hiyo isitishe kuipelekea Israel vifaa na vipuri vya ndege za kivita za F-35.

 
Kadhalika, wataalamu hao wa UN wamekaribisha hatua ya Ubelgiji, Italia, Uhispania, Uholanzi na kampuni ya Japan Itochu Corporation ya kusitisha kuupelekea silaha utawala haramu wa Israel.

Aidha wameyahimiza mataifa mengine kusitisha mara moja kuupelekea silaha utawala huo wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na leseni za usafirishaji na misaada ya kijeshi.

Japokuwa Umoja wa Ulaya umepunguza kasi ya uuzaji silaha kwa Israel, lakini Marekani imeendelea kuwa nchi inayoupelekea utawala huo wa Kizayuni silaha nyingi zaidi; na shehena za silaha zinazosafirishwa kutoka Washington kupelekewa Tel Aviv zimeongezeka zaidi tangu Oktoba 7, 2023.

Wapalestina wanaokaribia 30,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameshauawa shahidi hadi sasa kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghazza kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa Oktoba 7,2023 na wanamuqawama wa Palestina.../

Tags