Feb 28, 2024 06:46 UTC
  • Maduro akosoa jinai za kikoloni za Israel dhidi ya Palestina

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema jinai na mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza ni ishara ya wazi kuwa utawala wa Kizayuni unaendeleza malengo ya kikoloni dhidi ya Palestina.

Wizara ya Mawasiliano ya Venezuela imesema Rais Maduro amesema hayo katika kipindi cha 'Con Maduro Plus' na kueleza kuwa, Israel imeazimia kuudhibiti Ukanda wa Gaza na kulikoloni taifa la Kiarabu la Palestina, kwa namna inavyowashambulia kwa mabomu, kuwaua na kuwatendea jinai za kila namna Wapalestina.

Amesema: Mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina hayakubaliki. Israel inataka kulisambaratisha eneo lote la Ukanda wa Gaza ili ilikoloni kwa nguvu na mabavu.

Maduro amebainisha kuwa, nchi hiyo inaunga mkono kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, kuzidisha uingijizaji wa misaada ya kibinadamu na kutoa dhamana kwamba utawala wa Kizayuni utawajibishwa kwa jinai zake dhidi ya Wapalestina.  

Kadhalika Rais wa Venezuela amelaani kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa maangamizi ya kizazi yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusisitiza msimamo wa Caracas wa kutetea na kuunga mkono mapambano ya Palestina dhidi ya ubeberu wa Marekani.

Maduro: Jinai za Israel dhidi ya Palestina, zinafanana na jinai za Hitler dhidi ya Wayahudi

Maduro amesisitiza kuwa wananchi wa Palestina wana haki ya kupigania na kutetea ardhi yao ambayo imevamiwa na kughusubiwa kupitia vitendo vya mabavu na kupenda kujitanua vya utawala wa Israel.   

Mbali na kusisitiza kuwa Caracas inaunga mkono amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ya kuitaka Israel ichukue hatua za kukomesha mauaji ya kimbari Gaza, ameongeza kuwa, jinai za Israel kwa uungaji mkono wa Marekani ndizo zilizopelekea Aaron Bushnell, askari wa Jeshi la Anga la Marekani aliyekuwa na umri wa miaka 25, kujiua kwa kujichoma moto. 

 

Tags