Feb 29, 2024 07:13 UTC
  • Kabla ya kujichoma moto... Rubani Bushnell alifuchua:

Gazeti la New York Post limechapisha maelezo mapya kuhusu mwanajeshi wa Jeshi la Anga la Marekani, Aaron Bushnell ambaye alijichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington akipinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Gaza, na kumnukuu rafiki yake akisema kwamba Bushnell alimwambia ameona taarifa za siri zinazoonyesha ushiriki wa "vikosi vya jeshi Marekani katika kuua idadi kubwa ya Wapalestina.”

Kulingana na maelezo ya rafiki wa karibu wa rubani huyo wa Marekani ambaye jina lake halikuchapisha, Bushnell (25) alimfahamisha kwamba, alikuwa na kibali kinachomruhusu kutazama data za ujasusi za jeshi la Marekani zilizoainishwa kama " siri kuu."

Bushnell alikuwa akihudumu katika Kitengo cha 70 cha Ujasusi, Ufuatiliaji na Upelelezi wa Jeshi la Anga la Marekani, ambako inasemekana alifanya kazi kama "Fundi wa Huduma za Ubunifu."

Rafiki yake, ambaye gazeti la New York Post limethibitisha kuwa alikuwa na uhusiano mkubwa na Bushnell, amesema, "kazi yake halisi ilihusisha kuchakata data za kijasusi, ambazo baadhi zilihusiana na mzozo wa Israel huko Gaza."

Ameeleza kuwa Bushnell alimpigia simu usiku wa Jumamosi, Februari 24 - yaani, saa chache kabla ya kujichoma moto Jumapili mchana - na kumwambia kwamba baadhi ya habari alizoziona zilionyesha kuwa "jeshi la Marekani linahusika katika operesheni za mauaji ya kimbari zinazoendelea Palestina."

Aaron Bushnell

Aliendelea kusema kwamba: "Aliniambia Marekani imetuma vikosi vya nchi kavu, na kwamba wanaua idadi kubwa ya Wapalestina."

Pia ameeleza kuwa Bushnell alizungumza kuhusu wanajeshi wa Marekani wanaopigana kwenye mahandaki yanayotumiwa na makundi ya mapambano ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Jumatatu iliyopita, Aaron Bushnell alielekea katika ubalozi wa Israel mjini Washington ambako alijimwagia petroli kichwani na nguoni na kujichoma moto huku akikariri kwa sauti kubwa: “Palestina Huru, Palestina Huru” hadi alipokata pumzi. Rubani huyo shujaa mtetezi wa Wapalestina ambaye alisema kwa sauti kubwa kwamba hataki kushiriki tena katika mauaji ya kimbari, aliaga dunia baadaye.