Wosia wa Bushnell: Majivu ya mabaki yangu yamiminwe Palestina
Aaron Bushnell, afisa wa Jeshi la Anga la Marekani, ambaye alifariki dunia hivi karibuni baada ya kujichoma moto akipinga uungaji mkono wa nchi yake kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, aliandika katika wosia wake kuwa majivu ya mabaki ya mwili wake yamiminwe katika ardhi ya taifa huru la Palestina.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mafariki wa karibu wa Bushnell zilizochapishwa katika tovuti ya Crimethinc, askari huyo wa Jeshi la Anga la US aliandika wosia akitaka majivu na maiti yake yamiminwe katika ardhi ya Palestina.
Amesema kwenye wosia huo kuwa, "Iwapo muda utafika Wapalestina wadhibiti tena ardhi yao, na pia iwapo watu asilia wa ardhi hiyo (Palestina) wataafika wazo langu, ningelipenda majivu yangu yasambazwe katika Palestina iliyo huru."
Wosia wa askari huyo ambaye anaendelea kupongezwa na watu wa matabaka mbalimbali kwa kitendo chake cha kishujaa unaendelea kusema kwenya kuwa, "Sitamani majivu yangu yamiminwe popote pale (ghairi ya Palestina) kwa kuwa mwili wangu si milki ya sehemu yoyote ile duniani."

Bushnell ambaye alikuwa na umri wa miaka 25, alisikika akisema "Palestina Huru" wakati akijichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington D.C, katika tukio hilo la Jumapili iliyopita, ambalo limeendelea kuishangaza dunia nzima.
Kitendo chake hicho kimegeuka na kuwa moja ya nembo za mapambano ya ukombozi wa Palestina katika kona mbali mbali za dunia. Maveterani kadhaa wa kivita wa Marekani wameonekana kwenye picha na video zilizosambaa mitandaoni wakichoma moto magwanda yao kwa ajili ya kumuenzi afisa huyo wa Jeshi la Anga la Marekani.
Marekani imekuwa muungaji mkono mkubwa zaidi wa kisiasa, kijeshi na kijasusi wa vita vya mauaji ya kimbari ambayo utawala haramu wa Israel ulianzisha dhidi ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.