Baadhi ya Waislamu waanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani
Baadhi ya mataifa ya Kiislamu Jumatatu ya leo yameanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kanali ya Televisheni ya al-Alam imetangaza kuwa, baadhi ya mataifa ya Kiislamu yametangaza kuwa, Jumatatu ya leo tarehe 11 Machi ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya mataifa yaliyotangaza kuwa, leo ni Ramadhani Mosi ni Saudi Arabia, Qatar, Imarati, Lebanon, Palestina, Uturuki na Waislamu wa madhehebu ya Sunni nchini Iraq.
Waislamu wengine duniani wanatarajiwa kuanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani Jumanne ya kesho.
Baadhi ya mataifa yaliyotangaza kwamba, yataanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani kesho Jumanne ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Oman, Australia, Singapore, Indonesia, Malaysia na Brunei.
Ramadhani ni mwezi wa 9 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, mwezi wa baraka na ibada ambao ndani yake kiliteremshwa kitabu kitukufu cha Qur'ani.
Idhaa ya Kiswahilii ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawatakia Waislamu wote ulimwenguni Ramadhani Mubarak na funga njema pamoja na kutakabaliwa Saumu na ibada zao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.