Ureno yaibamiza Ufaransa na kutwaa Kombe la Yuro 2016
Timu ya taifa ya Ureno imefuta uteja wa takriban miongo 4 dhidi ya Ufaransa kwa kuisasambua bao 1-0 katika mchuano wa fainali ya Kombe la Yuro mwaka huu 2016 mjini Paris.
Ufaransa ambayo mara ya mwisho kufungwa na Ureno ilikuwa April 26 mwaka 1975 ilikubali kichapo cha bao 1-0 licha ya kwamba ilikua inaupiga nyumbani katika uwanja wa Stade de France katika kitongoji cha Saint-Denis, kaskazini mwa mji mkuu Paris. Fainali ya jana ilichezwa katika hali ambayo, wengi walikuwa wamebashiri kuwa mwenyeji Ufaransa ingeshinda kutokana na rekodi yake ya miaka 40 kutofungwa na Ureno. Nusra vijana wa Ureno wapoteze matumaini baada ya nahodha wao Cristiano Ronaldo kushindwa kuendelea na mchezo kutokana na jeraha la goti. Mchezo huo ulionekana kuwa mgumu licha ya Ufaransa kuongoza kwa kumiliki mpira kwa asilimia 54 kwa 46. Dakika 90 za ada zilimalizika kwa suluhu ya mtungi kwa mtungi, hivyo refa akalazimika kuongeza dakika 30 za ziada na hapo ndipo kitumbua cha Wafaransa kikaingia mchanga, kupitia goli la pekee la mtoka benchi Eder Antonio la dakika ya 109. Hii ni mara ya kwanza kwa vijana wa mkufunzi Fernando Santos kutwaa taji hilo na iwapo Ufaransa wangeshinda, wangekuwa tu wanaendeleza ubabe wao katika soka.