Apr 13, 2024 12:09 UTC
  • Ombi la Rais wa Marekani kwa Iran: Msiishambulie Israel

Rais wa Marekani kwa mara nyingine tena, katika uingiliaji wa wazi na kuunga mkono utawala wa Israel, ameiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isijibu mashambulizi ya utawala huo kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus huko Syria.

Jumatatu Aprili 1, 2024, ndege za kivita za Israel zilishambulia sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuua shahidi washauri saba wa kijeshi wa Iran. 

Kitendo hicho cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni wa Israel, kimelaaniwa na nchi nyingi za duniani.

Kwa msingi huo, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanasisitiza ulazima wa kuadhibiwa utawala wa Kizayuni kwa jinai hiyo na kutangaza kuwa Iran italipiza kisasi cha jinai hiyo.

Rais wa Marekani Joe Biden jana Ijumaa akizungumzia azma ya Iran ya kujibu shambulio la Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, kwa mara nyingine tena aliunga mkono utawala huo katili na kutangaza kuwa Marekani italinda usalama wa Israel na kuitetea.

Akijibi swali kuhusu ujumbe wake kwa Iran kuhusiana na jibu la mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kislamu  mjini Damascus, Joe Biden amesema: "Msifanye hivyo."

Wakati huo huo, Rais wa Marekani amesema: "Sitaki kufichua habari za siri, lakini matarajio yangu ni kwamba majibu ya Iran kwa mashambulizi ya Israel yatatokea hivi karibuni."

Sambamba na hayo, vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, tishio la Iran kulipiza kisasi shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo nchini Syria limeipoozesha na kuilemaza Israel kutokana na hofu kubwa.

Kutokana na hofu hiyo ya kulipiza kisasi, Israel imefunga balozi 28 katika nchi mbalimbali duniani.

Televisheni ya Israel imeonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza, kuna hofu ya shambulizi la moja kwa moja kutoka Iran dhidi ya Israel, na imenukuu vyanzo vya usalama kuwa Tehran "imedhamiria kujibu kuliko hapo awali."

Tags