Apr 23, 2024 11:32 UTC
  • Manyanyaso ya Waislamu, India
    Manyanyaso ya Waislamu, India

Chama cha Indian National Congress, ambacho ndicho kikubwa zaidi cha upinzani nchini India, kimewasilisha ombi kwa Tume ya Uchaguzi kikitaka kuchukuliwa hatua dhidi ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, kwa kutoa matamshi ambayo Congress inasema "hayakubaliki kabisa" dhidi ya Waislamu nchini humo na yanakiuka sheria za uchaguzi.

Ni baada ya Narendra Modi - ambaye anapigania kushinda muhula wa tatu mfululizo - kuwataja Waislamu kuwa nii "wapenyezaji" tu katika nchi ya India wakati wa hotuba yake aliyoitoa katika mojawapo ya kampeni zake za uchaguzi, Jumapili iliyopita, ambayo yamekosolewa na makundi ya upinzani.

Chama cha Wahindu cha  Bharatiya Janata cha Modi kinawashambulia Waislamu kwa viwango vyao vya juu vya uzazi na kuelezea hofu kwamba idadi ya Waislamu nchini India itazidi ya Wahindu waliowengi kwa sasa.

Narendra Modi

Idadi ya Waislamu nchini India inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 200, jambo ambalo linaifanya kuwa nchi ya tatu yenye Waislamu wengi duniani.

Kiongozi wa chama cha  Indian National Congress, Abhishek Manu Singhvi, amesema kauli ya Modi "haikubaliki kabisa" na inakiuka vifungu vya sheria ambavyo vinawakataza wagombea kuwahamasisha raia kupiga kura au kutopiga kura kwa mtu yeyote kwa msingi wa "dini", "kundi la kijamii" au "ishara za kidini".

Serikali ya India inayoongozwa na Narendra Modi imekuwa ikilaumiwa mara kwa mara kwa kutekeleza sera ya kibaguzi dhidi ya Waislamu; na mashirika ya kiraia, makundi ya upinzani na baadhi ya nchi za kigeni zimeelezea wasiwasi wao kuhusu maamuzi ambayo wanasema yanalenga kuchochea ubaguzi na kukibakisha chama cha Bharatiya Janata madarakani.