Apr 23, 2024 12:04 UTC
  • Tume ya Haki za Binadamu ya Ulaya: Uingereza isitishe mpango wa kuwapeleka wahamiaji huko Rwanda

Tume ya Kutetea Haki za Binadamu ya Ulaya, imetoa wito kwa Uingereza kutupilia mbali mpango wake wenye utata wa kuwatuma waomba hifadhi nchini Rwanda.

Wito huo umetolewa baada ya Bunge la Uingereza kupitisha muswada wenye utata unaoruhusu serikali kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi waliofika nchini Uingereza kinyume na utaratibu.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Baraza la Ulaya, Michael O'Flaherty, mpango huo wa serikali ya Kigali na Uingereza, unaibua maswali mengi kuhusu haki za waomba hifadhi na sheria kwa ujumla.

O'Flaherty ameelezea wasiwasi wake kwamba muswada huo unawezesha utekelezaji wa sera ya kuwaondoa watu kwenda Rwanda bila tathmini ya awali ya madai yao ya kuomba hifadhi kwa mamlaka ya Uingereza.

O'Flaherty pia ameonya kuwa muswada huo uliopasishwa na Bunge la Uingereza unazuia kwa kiasi kikubwa mahakama za Uingereza kuangazia kikamilifu na kwa uhuru maswala yanayowasilishwa mahakamani.

Mahakama ya Juu ya Uingereza ilisema mwaka uliopita kwamba, mpango wa serikali ya London wa kuwapeleka nchini Rwanda wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo unakiuka sheria. Ilisema mpango huo unawaweka katika hali hatarishi wakimbizi hao, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao waliikimbia nchi yao ya Rwanda, na kuwarejesha huko ni kutawaweka hatarini.