May 07, 2024 02:18 UTC
  • Janga la Mafuriko, maporomoko yaua watu 75 nchini Brazil

Kwa akali watu 75 wamepoteza maisha nchini Brazil baada ya kutokea janga kubwa la mafuriko.

Taarifa zaidi zinasema, mafuriko makubwa katika jimbo la kusini mwa Brazil la Rio Grande do Sul yamesababisha vifo vya watu 75 na wengine 103 hawajulikani walipo katika kipindi cha siku saba zilizopita.

Watu wasiopungua 155 wamejeruhiwa huku mafuriko hayo yakiwalazimisha zaidi ya watu 88,000 kuyakimbia makazi yao.

Mamlaka husika nchini Brazil zinasema kwamba watu wengine 16,000 wamepewa hifadhi kwenye majengo ya shule, kumbi za mazoezi na makaazi ya muda.

Mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku kadhaa yamesababisha kutokea maporomoko ya udongo, kusomba barabara na kuvunja madaraja ya jimbo hilo.

 

Baadhi ya maeneo hali ni mbaya huku barabara nyingi zikiwa hazipitiki kabisa. Aidha huduma za mawasiliano na umeme katika baadhi ya maeneo pia hazipatikani kutokana na athari mbaya iliyosababishwa na mafuriko hayo.

Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil alilitembelea jimbo hilo kwa mara ya pili siku ya Jumapili akiwa ameongozana na mawaziri kadhaa kukagua athari na uharibifu uliotokea katika maeneo hayo.

Wakati huo huo serikali ya Brazil imetangaza kuwa, inafanya kila awezalo kuwasaidia waathirika wa janga hilo la mafuriko na maporomoko ya udongo.