May 24, 2024 02:37 UTC
  • ICJ kutoa uamuzi wake kuhusu ombi la Afrika Kusini la kutaka Israel isitishe vita Gaza

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (OCJ) leo Ijumaa inatarajiwa uamuzi wake kuhusiana na ombi la Afrika Kusini la kutaka Israel kushinikizwa kutekeleza wito wa usitishwaji wa mapigano katika ukanda wa Gaza huko Palestina.

Taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo jana Alkhamisi ilibaini kwamba, leo ndio siku ya mahakama hiyo kutoa uamuzi kuhusu ombi la Afrika Kusini.

Pamoja na kuweko uamuzi wa mahakama ya ICJ, ambayo majaji wake wanatoa maamuzi kuhusu mizozo kati ya mataifa, haina uwezo wa kushinikiza utelezwaji wa maamuzi yake.

Uamuzi wa ICJ huenda ukaongeza shinikizo kwa Israel ambayo tayari mwendesha mashtaka wa ICC ameomba kibali cha kukamatwa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Katika shauri lake, Afrika Kusini imeitaka Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa iamuru kusitishwa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Rafah kama sehemu ya kesi yake iliyofungua mjini The Hague inayoushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mauaji ya kimbari, ikisema utawala huo "lazima uzuiwe" ili kunusuru maisha ya Wapalestina.

Majaji wa Afrika Kusini wakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ

 

Afrika Kusini inaushutumu utawala wa Kizayuni kwa vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Mnamo Januari, Mahakama ya ICJ iliamuru Israel ihakikishwe wanajeshi wake hawafanyi mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza, kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu na kuhifadhi ushahidi wowote wa ukiukaji wa hatua hizo, lakini utawala huo haujatekeleza agizo hata moja la mahakama hiyo.