Maelfu waandamana Kashmir kutoa heshima na kumuomboleza Shahidi Rais Raisi
Maelfu ya watu wameandamana katika eneo la Kashmir kutoa heshima zao na kuomboleza kifo cha marehemu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Shahidi Sayyid Ebrahim Raeisi, ambaye alikufa shahidi katika ajali ya helikopta pamoja na maafisa wengine kadhaa mapema wiki hii.
Katika upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Ustawi wa Taifa cha Afghanistan amesema, mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika mazishi ya rais wao aliyekufa shahidi ni ishara ya kushikamana kwao na Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu.
Mohammad Hassan Jafari, ameeleza hayo katika salamu za rambirambi alizotoa kufuatia ajali ya helikopta iliyopelekea kupoteza maisha Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa kadhaa.
Katika salamu zake hizo kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi na serikali ya Iran, Jaaafari ameongeza kuwa, mahudhurio makubwa ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali duniani katika shughuli ya kutoa heshima za mwisho nayo pia ni ishara ya hadhi na heshima maalumu iliyopewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akiashiria njama na kampeni zilizofanywa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran, Katibu Mkuu wa Chama cha Ustawi wa Taifa cha Afghanistan amesema, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vilijaribu kuchochea ili mahudhurio ya wananchi wa Iran katika mazishi ya Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na maafisa wengine wa Iran yawe ya kiwango cha chini, lakini mamilioni ya watu walihudhuria mazishi na shughuli ya kuusindikiza mwili wa rais wao aliyekufa shahidi.../