ICJ yaiamuru Israel isimamishe mashambulio yake Rafah, Ghaza
Mahakama ya Umoja wa Mataifa imeuamuru utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake katika mji wa kusini mwa Ghaza wa Rafah na kujiondoa katika eneo hilo, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ikiishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari, na kuielezea hali hiyo kuwa ni hatari kubwa kwa wakazi wa Palestina.
Uamuzi huo uliotangazwa leo Ijumaa na Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya
Haki (ICJ) umekuwa ni wa tatu kutolewa mwaka huu na jopo la majaji 15 ambalo
limetoa maagizo ya awali ya kutaka kudhibitiwa ongezeko la idadi ya vifo na
kupunguza mateso ya kibinadamu huko Ghaza. Ingawa amri za ICJ zina nguvu
kisheria, lakini mahakama hiyo haina vyombo vya kulazimisha utekelezaji wake.
Akisoma uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki au Mahakama ya Dunia,
Rais wa Jopo la Majaji, Nawaf Salam, amesema hatua za muda zilizoamriwa na
mahakama hiyo mwezi Machi hazijashughulikia kikamilifu hali ya eneo la Palestina
linalozingirwa hivi sasa, na hali ya sasa imeweza kuzingatiwa ipasavyo kwa agizo
jipya la dharura lililotolewa.
Jaji Salam amesema Israel lazima ikomeshe mara moja mashambulizi yake ya
kijeshi, na hatua nyingine yoyote katika eneo la Rafah, ambayo inaweza
kusababishia kundi la Wapalestina huko Ghaza hali ya maisha ambayo inaweza
kuleta uharibifu wa kimwili kwa ujumla wao au kwa baadhi yao; na kuielezea hali
ya kibinadamu katika mji wa Rafah kuwa ni ya "janga".
Wiki iliyopita, Mawakili wa Afrika Kusini waliitaka mahakama ya ICJ yenye makao
yake mjini The Hague kuchukua hatua za dharura, wakisema mashambulizi ya
utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Rafah lazima yakomeshwe ili kuhakikisha
usalama wa maisha ya Wapalestina…/