Ripoti: Chuki dhidi ya Waislamu Austria zimefikia kiwango cha juu
Austria imerekodi idadi kubwa zaidi ya matukio ya chuki dhidi ya Uislamu katika mwaka uliopita wa 2023 tangu ilipoanza kuweka rekodi za matukio hayo mwaka 2015.
Ripoti ya Kituo cha Nyaraka kuhusu chuki dhidi ya Uislamu na Ubaguzi dhidi ya Waislamu nchini Austria imeendelea kubainisha kuwa Waislamu wamedunishwa na kuvuliwa utu wao kwa kulinganishwa na wanyama katika maoni mbalimbali ya hisia za chuki yaliyotolewa mitandaoni.
Watu wengi waliotoa maoni hayo ya chuki waliwahusisha Waislamu peke yao na tuhuma za kueneza chuki dhidi ya Wayahudi.
Katika ripoti yake hiyo, kituo hicho cha nyaraka cha Austria kimesisitiza kuwa takwimu ilizotoa ni muhtasari tu wa matukio, lakini idadi halisi ya kesi hizo inaaminika kuwa kubwa zaidi.
Ripoti hiyo imemalizia kwa kutoa indhari kwamba takwimu hizo "ni hali ya kutia wasiwasi" juu ya mambo yanayochangia zaidi mgawanyiko na mpasuko katika jamii na kutaka kushughulikiwa kwa umakini zaidi tatizo la uenezaji chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.../