Jun 07, 2024 02:45 UTC
  • Mkuu wa NATO: Hatutatuma wanajeshi Ukraine

Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO amesema muungano huo wa kijeshi wa Wamagharibi hauna mpango wa kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine.

Jens Stoltenberg alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari akiwa ziarani Finland akiwa pamoja na rais wa nchi hiyo, Alexander Stubb na kusisitiza kuwa, NATO haina mpango wa kutuma vikosio vyake Ukraine, na kwamba jumuiya hiyo ya kijeshi haiitazami Russia kama tishio la kijeshi kwa nchi za Magharibi. 

Rais Stubb pia amesisitiza kuwa, Finland haina mpango wa kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine na badala yake, inatafakari kuhusu machaguo mengine kadhaa, kama vile kuipa Kiev msaada wa kifedha, kijeshi au silaha.

Msimamo wa NATO umekuja siku chache baada ya Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary kuonya kuwa, shirika hilo la kijeshi la Magharibi linakaribia kutuma askari wake huko Ukraine.

Alitahadharisha kuwa, EU inachezea moto kwa sababu vita kati ya Russia na Ukraine ni kinamasi ambacho kinaweza kuivuta Ulaya katika kina chake kirefu.

Vita vya Ukraine na Russia

Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya nchi za Magharibi  zinataka kutumwa askari wa NATO nchini Ukraine, lakini zingine zinasisitiza kuwa haziungi mkono mpango huo zikionya kuwa, hatua hiyo inaweza kuzusha Vita vya Tatu vya Dunia.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekuwa akiwashinikiza viongozi wa Magharibi waipe Kiev silaha na vifaa zaidi vya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Moscow.

Tags