Juhudi za BRICS za kutumia sarafu za taifa katika mabadilishano ya kibiashara
Nchi wanachama wa kundi la BRICS zinafanya jitihada kubwa za kuhakikisha zinakuwa na mfumo maalumu wa mabadilishano ya kibiashara kwa kutumia sarafu za taifa za nchi wanachama.
Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa wanachama BRICS wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanatekeleza kivitendo maamuzi yaliyochukuliwa kwenye kikao cha mwaka jana cha kundi hilo mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Amesema hayo kwenye kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa BRICS kilichofanyika nchini Russia na kusisitiza kuwa, wanachama wa kundi hilo wana nia ya kweli ya kuanzisha mfumo maalumu wa mabadilishano yao ya kibiashara kwa kutumia fedha za taifa za nchi wanachama.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa, kupambana na ukiritimba wa sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi wanachama wa BRICS kuna manufaa kwa pande kadhaa. Mosi ni kwamba jambo hilo linazidisha uhuru wa kundi hilo katika maamuzi yake hasa ya kiuchumi. Pili jambo hilo litaipelekea kila nchi mwanadhama wa BRICS kupunguza mno kutegemea Magharibi na kujiepusha na hatari za kifedha zinazosababishwa na utegemezi huo. Na tatu jambo hilo litafanikisha malengo ya BRICS ya kujiweka mbali na madola ya Magharibi na kutia nguvu madola ya Mashariki mwa dunia. Mohsen Rui Sefat, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: “Ni jambo lisilo na shaka kwamba moja ya shabaha kuu za BRICS ni kutia nguvu madola ya Mashariki mbele ya madola ya Magharibi na moja ya mambo ya lazima kabisa ya kufanikisha jambo hilo ni kupunguza kutumia sarafu za madola ya Magharibi katika mabadilishano yao ya kibiashara.”

Tab’an juhudi za kupambana na ukiritimba wa sarafu ya dola zilianza zamani, na kinachofanywa na kundi la BRICS hivi sasa ni kutia nguvu tu jitihada hizo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, nchi wanachama wa kundi hilo wameshadidisha jitihada zao za kutekeleza kivitendo maamuzi wa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa BRICS uliofanyika mwaka jana huko Johannesburg, Afrika Kusini hususan suala la kutia nguvu mfumo wa mabadilishano ya biashara kwa kutumia sarafu ya kila nchi mwanachama. Amesema, karibuni hivi nchi wanachama wa BRICS zitaweza kutumia kikamilifu sarafu za nchi zao katika mabadilishano ya kibiashara baina yao, jambo ambalo bila ya shaka yoyote litazidisha thamani ya sarafu hizo.
Kwa kutilia maana kwamba, kadiri siku zinavyopita ndivyo nafasi ya sarafu ya dola inavyozidi kudhoofika duniani. Hii ina maana kwamba, kutumiwa sarafu za kitaifa katika mabadilishano ya kibiashara kutazuia kudharauliwa sarafu ya nchi yoyote ile na wakati huo huo kutaizuia Marekani kutumia sarafu yake ya dola kama silaha za kuzishinikiza nchi nyingine katika miamala ya kibiashara na mahusiano ya kiuchumi na kifedha bali hata katika masuala ya kiusalama. Tunaweza kusema pia kuwa, kundi la BRICS limefanya jambo la busara sana kuamua kutumia sarafu za nchi wanachama kwenye mabadilishano ya kibiashara hasa katika kupambana na ukiritimba wa madola ya Magharibi katika masuala ya kifedha ulimwenguni.

Vile vile kuna uwezekano Marekani ikaamua kutumia sarafu yake ya dola kulishinikiza kundi la BRICS. Hivyo uamuzi wa kundi hilo wa kutumia sarafu za taifa za nchi wanachama, utaipoka Marekani silaha ya kutumia sarafu ya dola dhidi ya kundi hilo. Sarafu ya dola kama tulivyoona, ni miongoni mwa nyenzo zinazotumiwa na Marekani kueneza ubeberu wake duniani, hivyo hatua yoyote ile itakayopelekea kupungua matumizi ya sarafu hiyo ni muhimu, kwani itadhoofisha ubeberu wa Marekani na kusaidia kuleta uadilifu ulimwenguni.