Jul 12, 2024 03:04 UTC
  • Putin: Huenda BRICS ikaunda Bunge lake katika siku zijazo

Rais Vladimir Putin amedokeza kuwa, yumkini kundi la BRICS la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani likaunda Bunge lake katika mustakabali wa karibu.

Akihutubia washiriki wa duru ya 10 ya Jukwaa la Kibunge la BRICS mjini St. Petersburg nchini Russia, Putin amesisitiza kuwa, mikutano ya mara kwa mara ya wabunge wa nchi wanachama wa BRICS itaharakisha mchakato wa kuundwa Bunge la jumuiya hiyo.

Ameuhutubu mkutano huo kwa kusema: BRICS kwa sasa haina muundo wa kitaasisi wa Bunge, lakini naamini wazo hili litaafikiwa karibuni. Naamini jukwaa lenu litakuwa na mchango mkubwa katika hili.

Rais Putin amekutana na kufanya mazungumzo na Maspika wa Mabunge ya China na Tanzania, Zhao Leji na Tulia Ackson, pambizoni mwa mkutano huo wa Jukwaa la Kibunge la BRICS mjini St. Petersburg.

Kundi hili la BRICS ambalo hadi hivi karibuni lilikuwa na wanachama wakuu watano tu, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, lililipanuka zaidi Januari mwaka huu baada ya Iran, Ethiopia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu kujiunga na kundi hilo.

Hali kadhalika, mataifa mengine mengi yakiwemo ya Afrika, Asia, na Amerika ya Latini yameonyesha nia ya kujiunga na BRICS, huku mengine yakiwa tayari yameshatuma maombi rasmi.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BRICS kwa sasa inachangia kiasi cha 36% ya Pato la Ghafi la Kimataifa katika suala la usawa wa uwezo wa kununua (PPP), ikilinganishwa na takribani 30% ya kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi. Aidha nchi za BRICS zinamiliki asilimia 25 ya biashara ya kimataifa, na asilimia 40 ya uzalishaji wa mafuta.

Tags