WFP: Watu milioni mbili wanataabika na njaa Gaza
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa zaidi ya watu milioni mbili katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na njaa kali, huku wengi wao wakikaribia kukumbwa na ukame na ukata wa ajabu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesisitiza katika taarifa yake kwamba, ukosefu wa usalama na machafuko katika eneo hilo (ambao unasababishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel) vitasalia kuwa changamoto kubwa iwapo msaada wa chakula hautafika Gaza. Shirika hilo limetoa wito wa kuongezwa kwa msaada wa chakula na kuharakishwa kwa usambazaji wake katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa ya Mpango wa Chakula Duniani imesema: "Palestina imekuwa ikikabiliwa na mzozo tata na wa muda mrefu wa kibinadamu na ulinzi kwa miongo kadhaa, mgogoro ambao unasababishwa na kuendelea kukaliwa kwa mabavu, migawanyiko ya kisiasa ya ndani na migogoro ya mara kwa mara, na ni tishio la mara kwa mara kwa utulivu na maendeleo ya watu wa Palestina."
Shirika hilo limeonya kuwa Gaza iko hatarini kukumbwa na njaa huku ghasia zikiendelea, vivuko vya mpakani vikiendelea kufungwa, na uhaba wa chakula ukiwa mkubwa. Kulingana na Mpango wa Chakula Duniani, maghala yake yamekuwa tupu tangu mwisho wa Machi, kwani vivuko vilikuwa vimefungwa tangu mwanzoni mwa mwezi huo.
Ripoti hiyo inatolewa katika hali ambayo, asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimeendelea kutoa indhari kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoukabili Ukanda wa Gaza na kutaka kuchukuliwa hatua za kukomesha uzuiaji wa upelekaji wa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.