Maduro: Hatutakubali Venezuela iangukie mikononi mwa mafashisti
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema taifa hilo katu halitaruhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe viripuke nchini humo, huku akizikosoa vikali nchi za Magharibi kwa kuchochea vurugu na ghasia zinazoendelea kushuhudiwa nchini humo baada ya uchaguzi wa rais.
Katika kikao na waandishi wa habari akiwa katika Kasri ya Miraflores huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela, Rais Maduro sambamba na kuonya kuwa serikali yake haitaruhusu kuendelea ghasia na uhalifu nchini humo, amesema hawataruhusu nchi hiyo itumbukie mikononi mwa mabeberu, mafashisti, na wahalifu.
Ameeleza bayana kuwa, "Tunataka kila kitu kiwe ndani ya mfumo wa katiba. Hatutaki kutumia njia nyingine za kufanya mapinduzi."
"Uchumi wa nchi umekuwa ukilengwa, Venezuela haitaanguka katika mikono ya ubeberu, ufashisti na wahalifu," amesisitiza Rais Maduro, huku akizionya vikali nchi za Magharibi dhidi ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Amebainisha kuwa, misimamo ya nchi za Magharibi kuhusu uchaguzi wa rais wa Venezuela ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo, akisisitiza kuwa taifa hilo lina haki ya kuchukua hatua za kisiasa na kisheria ili kulinda haki na mamlaka yake ya kujitawala.
Tume ya Uchaguzi ya Venezuela ilitangaza kuwa Maduro ameshinda uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa kupata 51.2% ya kura, katika uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 28. Mkuu wa tume hiyo Elvis Amoroso amesema, Maduro mwenye umri wa miaka 61 amejipatia asilimia 51.2 ya kura, akimshinda mgombea wa upinzani Edmundo González, ambaye alipata asilimia 44.2.