NAM: Mauaji ya Ismail Haniyah ni kitendo cha kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i114936-nam_mauaji_ya_ismail_haniyah_ni_kitendo_cha_kigaidi
Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) sanjari na kulaani mauaji ya kigaidi ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Kisiasa wa Harakati ya Muqawama ya Palestina HAMAS, imeyataja mauaji hayo kama kitendo cha kigaidi.
(last modified 2024-08-07T06:51:45+00:00 )
Aug 07, 2024 06:51 UTC
  • NAM: Mauaji ya Ismail Haniyah ni kitendo cha kigaidi

Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) sanjari na kulaani mauaji ya kigaidi ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Kisiasa wa Harakati ya Muqawama ya Palestina HAMAS, imeyataja mauaji hayo kama kitendo cha kigaidi.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na NAM imebainisha kuwa, mauaji ya kigaidi ya Haniyah ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na ukanyagaji wa mamlaka ya kujitawala Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

NAM imeeleza bayana katika taarifa hiyo kuwa: Kitendo hiki cha kigaidi ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa zikiwemo haki za binadamu za kimataifa hususan haki ya kuishi na misingi iliyomo katika Hati ya Umoja wa Mataifa, na mamlaka na ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Imesisitiza kuwa, mauaji ya viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari, na raia wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na nchi nyingine za eneo, ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa, na inazuia juhudi za kidiplomasia za usitishaji vita wa kudumu na endelevu huko Gaza.

Marhum Ismail Haniyah

Jukwaa hilo kubwa zaidi duniani limesema kuwa, vitendo vya uhalifu vinavyolenga kutisha jamii, kikundi au watu maalumu kwa sababu yoyote ile, mahali popote na kwa mtu yeyote yule, haviwezi kuhalalishika kwa hali yoyote ile.

Aidha NAM imesisitiza katika taarifa hiyo kuwa, kuendelea mashambulizi ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza, kunapaswa kulaaniwa. Taasisi hiyo yenye wanachama 120 imeitaka jamii ya kimataifa izuie mauaji hayo ya kimbari Gaza na kuchukua hatua zote muhimu za kukomesha ukatili huo.