CAIR yamtaka Biden 'alaani' ugaidi wa kiserikali wa Israel
(last modified Sun, 11 Aug 2024 07:34:12 GMT )
Aug 11, 2024 07:34 UTC
  • CAIR yamtaka Biden 'alaani' ugaidi wa kiserikali wa Israel

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limemtaka Rais Joe Biden wa nchi hiyo ajibu na kulaani vitendo vya ugaidi wa kiserikali vinavyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

CAIR imesema katika taarifa kuwa, shambulio la Israel dhidi ya shule katika jiji la Gaza sio hujuma dhidi ya Wapalestina tu, bali ni shambulio dhidi ya dini, hasa kwa kuwa lilifanywa wakati wa Swala ya Alfajiri.

Baraza hilo la Waislamu wa Marekani limesema: Iwapo Rais Biden anajali chochote juu ya uhai wa mwanadamu, anapaswa kutoa jibu dhidi ya kitendo hiki cha ugaidi wa kiserikali na kuacha kuupelekea silaha utawala wa Kizayuni, na pia kumlazimisha (Benjamin) Netanyahu akubali makubaliano ya usitishaji vita ambao amekuwa akiyakanyaga.

Kadhalika kundi hilo la kutetea haki za Waislamu na kiraia nchini Marekani limeeleza kusitikishwa na hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza, na kusisitiza kuwa jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusimamisha mauaji ya watoto katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa. 

Nembo ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) 

Taasisi na nchi mbali mbali duniani zimeendelea kulaani jinai ya jana Jumamosi iliyofanywa na Israel dhidi ya Waislamu waliokuwa katikati ya Swala ya Alfajiri bila ya silaha bali kwenye mazingira ya kiraia kikamilifu katika shule ya al-Tabieen katika mji wa Gaza.

Algeria imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liitishe mkutano wa dharura wa kuchunguza na kujadili na kulaani jinai hiyo mpya ya utawala katili wa Israel katika Ukanda wa Gaza.