Putin aamua kusimamisha kikamilifu mazungumzo na Ukraine baada ya Kyiv kuivamia Russia
Rais Vladimir Putin wa Russia ameamua kusimamisha kikamilu mazungumzo na Ukraine baada ya nchi hiyo kushambulia taasisi za nyuklia za Russia.
Rais Putin amesema kuwa, kuanzia sasa majibu ya Russia yatakuwa makali zaidi na atahakikisha wanajeshi wa Ukraine waliovamia ardhi ya Russia, wote wanatimuliwa.
Wiki iliyopita, jeshi la Ukraine lilifanya shambulizi la kushitukiza katika eneo la Kursk nchini Russia suala ambalo limeliweka katika hali ya hatari zaidi jeshi la Ukraine kutokana na kudhoofika sana katika vita na pia kutokana na kwamba sasa Russia itakuwa inajibu uvamizi uliofanywa na wanajeshi hao wa Ukraine. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, Russia itaanzisha mashambulizi mengine makali dhidi ya wanajeshi wa Ukraine, karibuni tu hivi.
Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema Jumapili kwamba, mashambulizi ya kivamizi ya Ukraine dhidi ya Russia hayatoachwa vivi hivi hivi bila ya majibu makali.
Ukraine ilitumia makombora na ndege zisizo na rubani kushambulia maeneo hayo ya Russia na kuharibu miondombinu ya kiraia.
Baada ya matamshi hayo ya Zakharova, Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kutokuweko tena mazungumzo ya amani kati ya nchi yake na Ukraine, suala ambalo linaashiria kwamba karibuni hivi Moscow itatoa majibu makali dhidi ya wanajeshi wa Ukraine waliovamia ardhi ya Russia.