Aug 15, 2024 02:45 UTC
  • Japan yasema itaitambua Palestina kwa 'njia kamilifu'

Serikali ya Japan imesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, inatathmini suala la kulitambua rasmi taifa huru la Palestina.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Japan wamesema katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu kwamba, nchi hiyo inatafakari mpango wa kulitambua rasmi taifa huru la Palestina kwa 'njia ya kina na kamili.'

Maafisa hao wameiambia Anadolu katika mahojiano yaliyochapishwa jana Jumatano kuwa, nchi hiyo inatafakari mpango wa kulitambua rasmi taifa huru la Palestina, kwa kuzingatia maendeleo ya kile kinachoitwa mchakato wa amani wa Asia Magharibi.

"Japan inaendelea kuunga mkono 'suluhisho la serikali mbili' kupitia mazungumzo kati ya pande zote," wameeleza maafisa hao wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan na kuongeza kuwa: Tokyo ingependa kuwa na mchango katika mchakato wa amani kwa kutumia vyema nafasi ya kipekee ambayo Japan inayo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mwezi uliopita pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoko Kamikawa alisema nchi yake 'inaelewa' azma ya Wapalestina ya kutaka kuwa na nchi huru, na kwamba inaunga mkono 'suluhisho la kuundwa madola mawili' kama suluhu ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa miongo kadhaa wa Palestina na Israel.

Azma ya Japan ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Palestina kama sehemu ya kutekeleza jukumu lake katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) inakuja huku kukiwa na ongezeko la idadi ya mataifa ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Uhispania, Norway, pamoja na Ireland, kuitambua Palestina kama taifa huru.

Tags