Aug 15, 2024 13:21 UTC
  • Erdogan: Muundo wa Baraza la Usalama ufanyiwe mabadiliko ya kimsingi

Rais Recep Tayyib Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao uko mbali na utekelezaji majukumu yake ya kuhakikisha amani na usalama vinatawala duniani, lazima ufanyiwe mabadiliko ya kimsingi.

Rais wa Uturuki ameunga mkono kauli ya hivi karibuni za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama na kusisitiza haja ya kuwa na mfumo wa haki zaidi duniani.

Rais wa amemhutubu Guterres kwa kusema, Baraza la Usalama lilibuniwa na washindi wa Vita vya Pili vya Dunia. Ni jambo la thamani sana kueleza maoni yako kwa uaminifu na kwa sauti kubwa kuhusu ulazima wa kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulingana na hali ya sasa na kwa njia ya haki kwa ulimwengu kufurahia mfumo wa haki.

Ukumbi wa mikutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Akizungumzia Afrika kutokuwa na mwanachama wa kudumu katika baraza hilo Rais Erdogan amesema: Bara la Afrika na ndugu zetu wote wa Afrika wanapaswa kupewa fursa ya kushiriki katika mfumo huu wa haki, bado tunasema kwamba dunia ni kubwa kuliko mataifa matano.

 Ukosoaji wa muundo wa Baraza la Usalama umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni na kumekuwa kukitolewa wito wa kupanuliwa baraza hilo  ili kutoa uwakilishi zaidi kwa nchi za Asia, Afrika na Amerika Kusini na kuvunja udhibiti Wa nchi za Magharibi duniani.