Wabunge wa Ireland wataka Israel iwekewe vikwazo
Wabunge katika Jamhuri ya Ireland kwa kupasishwa hoja katika bunge la nchi hiyo, wameitaka serikali yao kuuwekea vikwazo utawala haramu wa Israel kutokana na mauaji yake dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA likinukuu vyanzo vya habari, wabunge wa Ireland wameishutumu Israel na kuutaja kama "utawala wa kihalifu" kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza.
Azimio hilo llimeitaka serikali kuiwekea Israel vikwazo vya kibiashara, usafiri na hata vya kidiplomasia ili kukabiliana na ukatili wake dhidi ya Wapalestina.
Watunga sheria hao wameitaka serikali yao kusitisha mara moja makubaliano ya kijeshi na silaha na Israel, kutangaza miamala yote ya kibiashara kuwa haramu, na kupiga marufuku matumizi ya anga ya Ireland na viwanja vya ndege kwa ndege zinazobeba silaha kwenda Tel Aviv.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Micheál Martin alifichua nia ya nchi yake ya kujiunga na faili la kisheria la Afrika Kusini dhidi ya Israel juu ya mauaji ya kimbari ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Aidha haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Ireland kuthibitisha kwamba, Jilan Wahba Abdul-Majid ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Ujumbe wa Palestina nchini Ireland ameteuliwa kuwa balozi wa Palestina kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo ya bara Ulaya.