Marekani yapinga tena azimio la kusitisha mapigano Gaza
Ikiwa ni katika muendelezo wa uungaji mkono wake mkubwa kwa utawala ghasibu wa Israel, mapema siku ya Jumatano Novemba, Marekani ilipinga tena rasimu ya azimio la wanachama 10 wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililotaka usitishaji vita wa mara moja, usio na masharti na wa kudumu huko Gaza na kuachiliwa huru mateka wote.
Katika kikao cha kupiga kura kuhusu rasimu ya azimio hilo, wajumbe 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio la kusitisha mapigano huko Gaza. Hakuna hata mmoja wa wajumbe wa Baraza la Usalama aliyepiga kura dhidi ya azimio hilo, lakini Marekani ikatumia kura yake ya turufu kulipinga, ambapo nchi wanachama 10 wa Baraza la Usalama ambazo ni Algeria, Ecuador, Japan, Msumbiji, Malta, Korea Kusini, Sierra Leone, Slovenia, Uswisi na Guyana ziliwasilisha rasimu ya azimio hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Robert Wood, balozi na naibu mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, amehalalisha kura ya turufu ya nchi yake dhidi ya azimio hilo kwa kudai kuwa Marekani haiwezi kuunga mkono usitishaji vita usio na masharti yoyote likiwemo la kuachiliwa huru mateka wa Israel.
Msimamo huo wa Marekani ambao umejikita katika uungaji mkono wa pande zote kwa utawala wa Kizayuni licha ya jinai zake hususan mauaji ya kimbari huko Gaza na pia kuchukuliwa kuwa ni taa ya kijani kwa ajili ya kuendelea mashambulizi na jinai za utawala huo ghasibu huko Gaza na hata nchini Lebanon, umekabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa nchi zingine za dunia. Majid Bamya, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amekosoa vikali kura ya turufu iliyopigwa na Marekani dhidi ya azimio hilo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mapema siku ya Jumatano na kusisitiza kuwa, hakukuwepo na uhalali wowote wa kupinga azimio hilo la kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel, kwa kuwa Israel daima itaendelea kudai kuwa masharti hayajatimizwa kwa sababu mipango yake ni kuendelea vita ili ipate fursa ya kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina na kufanya mauaji ya umati ya kuwatokomeza Wapalestina.
Vasily Nebenzya, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amesema kufuatia kura ya turufu ya Marekani dhidi ya azimio la usitishaji vita katika Baraza la Usalama, kwamba Marekani inahusika pakubwa na mauaji ya Wapalestina. Ameendelea kusema kuwa uvurugaji huo wenye nia mbaya na ambao unafanywa kwa utulivu kamili wa Marekani dhidi ya takwa dogo na la kawaida kabisa la Baraza la Usalama kwa ajili ya kuokoa maisha ya binadamu ni kitendo cha kikatili na unyama wa hali ya juu.
Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa pia amesema hivi katika hotuba yake: "Matumizi ya kura ya turufu ya Marekani dhidi ya usitishaji vita yamesambaratisha kabisa matarajio ya watu wa Gaza, na kamwe historia haitasahau jambo hilo." Mwanadiplomasia huyo wa China ameongeza kuwa Marekani inaendelea kutuma silaha Israel na licha ya njaa kali inayowakodolea macho watu wa Gaza, bado inaendelea kuhalalisha hatua zake hizo za kidhalimu dhidi ya watu wasio na hatia. Amesema, Israel imekiuka mistari myekundu na sheria zote za kimataifa ambapo imeua zaidi ya watu 44,000 huko Gaza, lakini pamoja na hayo Marekani haijasita kutumia kura yake ya turufu kupinga usitishaji vita.
Azimio la Baraza la Usalama kuhusu Gaza lilisisitiza kufuatiliwa mihimili mitatu ambayo ni "kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza wakati wa mwezi wa Ramadhani, kuachiliwa mara moja mateka wote bila masharti na kuruhusiwa kuingia misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Nukta muhimu ya kuzingatiwa hapa ni kwamba licha ya Israel kukataa kukubali matakwa ya jamii ya kimataifa, lakini utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani unaendelea kutoa uungaji mkono mkubwa wa hali na mali wa kisiasa na kijeshi kwa utawala huo wa Kizayuni na umekuwa ikitoa tu maneneo matupu yasiyo na maana yoyote na wakati huo huo kujiepusha kutoa mashinikizo yoyote ya kisiasa, kijeshi na kifedha dhidi ya utawala huo katili.