Araghchi: Kila nchi ina haki halali ya kujilinda
(last modified Sun, 15 Jun 2025 08:00:10 GMT )
Jun 15, 2025 08:00 UTC
  • Araghchi: Kila nchi ina haki halali ya kujilinda

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: Kila nchi ina haki halali ya kujilinda na kujihami mbele ya uchokozi.

Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo mapema leo katika kikao na mabalozi na wakuu wa ujumbe wa kigeni na wa kimataifa wanaoishi mjini Tehran na kuongeza kuwa, nchi nyingi za eneo hili zimelaani hujuma dhidi ya Iran na vituo vyake nyuklia na kusema: Ninawashukuru mabalozi na nchi zote za eneo hili zilizolaani jinai hiyo ya Israel.

Amma kuhusu majibu ya Iran kwa ugaidi huyo wa Israel, Araghchi amesema: Hivi ndivyo vikosi vyetu vya ulinzi vilivyoanza kutoa majibu siku mbili zilizopita na vitaendelea.

Waziri Araghchi amesema: Tumo katika kujibu mashambulizi haya kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Ni haki halali ya kila nchi kujilinda mbele ya uchokozi na ndivyo jeshi letu lilivyoanza kujihami tangu siku mbili zilizopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Hatutaki vita hivi vienee katika nchi nyingine au kwenye ukanda huu kwa njia yoyote, isipokuwa tutakapolazimishwa kujibu uchokozi. Kimsingi, hatukuanzisha vita hivi na tulikuwa tukifuata mkondo wa kidiplomasia kuhusu mpango wetu wa amani wa nyuklia, na leo Jumapili ilikuwa niende Muscat Oman kushiriki kwenye duru mpya ya mazungumzo lakini tumechokozwa na ndio maana tunajibu. Tunajitetea na kujihami huku ni halali kabisa.