Chuki dhidi ya Uislamu Magharibi zimeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa
Dec 15, 2024 05:34 UTC
Washiriki wa mkutano wa London uliozungumzia "Uenezaji Hofu na Chuki Dhidi ya Uislamu" (Islamophobia) wametahadharisha kuhusu athari za vita vya Ghaza kwa ongezeko la jinai zinazofanywa katika nchi za Magharibi kwa sababu ya kuwachukia Waislamu.
Dawud Walid, Mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) na mjumbe wa Baraza la Maimamu wa Jamii ya Michigan nchini Marekani, amesema katika mkutano wa London uliochunguza uenezaji chuki dhidi ya Uislamu kwamba, takwimu zinaonyesha kuwa, jinai zilizofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na baada ya Oktoba 7 ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa zimeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Mkuu wa CAIR amedokeza kuwa, takwimu za uhalifu uliofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu huko Michigan ni za kiwango cha juu zaidi kuliko zilizofanywa ndani ya Marekani yote, na akasema, tatizo hilo limetokana na uenezaji chuki dhidi ya Wapalestina unaofanywa na wanasiasa na vyombo vya habari.

Mwandishi na mwanaharakati wa kiraia Sandew Hira, yeye ameliezea suala la uenezaji chuki dhidi ya Uislamu kama ishara ya hofu iliyoipata Magharibi kutokana na kuenea Ustaarabu wa Kiislamu unaotazamwa kama simulizi mbadala.
Anne Norton, Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania, yeye amesema, sera ya uenezaji chuki dhidi ya Uislamu katika jamii za Magharibi imegonga mwamba, na akabainisha kuwa, kutokana na kuongezeka idadi ya Waislamu katika muongo uliopita, wao sasa wamekuwa kundi lenye ushawishi katika nchi za Magharibi.
Mwenendo ulioratibiwa wa kueneza chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya ungali unaendelea; na moja ya matokeo na athari zake ni kushadidi tabia za kibaguzi, upendeleo na ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii ya Waislamu katika bara hilo.../
Tags