UNICEF yataka kulindwa watoto wakimbizi
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeeleza kuwa watu 2,275 mwaka jana walipotea katika bahari ya Mediterania na kwamba aghalabu yao wanaaminika kuwa walipoteza maisha katika njia hatari za bahari hiyo khususan zile zinaoztumiwa na wafanya magendo ya binadamu kutoka Tunisia na Libya kwa lengo la kufika Italia.
Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeeleza kuwa watoto wadogo ni miongoni mwa raia wanaokimbia nchi zao. Limesema kuwa, mwaka jana, watu 60,000 waliwasili Italia wakiwemo watoto 8,000 wasio na wazazi wala jamaa.
Andrea Lacomini Msemaji wa UNICEF amesema kuwa wakimbizi hawa tajwa mara nyingi huwa wanakimbia vita, mapigano na umaskini mkubwa. Huwa ni mabinti na wavulana wanaowakilisha asilimia 20 ya watu wanaowasili Italia.
Shirika la UNICEF linazitolea wito serikali mbalimbali kutoa kipaumbele kwa suala la ulinzi kwa wakimbizi watoto. Haivumiliki kuona mtoto anapoteza maisha baharini, kuona mtoto anamshuhudia mama yake akipoteza maisha na hadi sasa tumeshuhudia kesi nyingi za aina hii.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia imeeleza kuwa, mwaka jana wahamiaji 66,317 waliwasili nchini humo kwa njia ya bahari; kiwango ambacho ni chini ya nusu ikilinganishwa na mwaka 2023.