Trump akosolewa kwa kuirejesha Ansarullah katika 'orodha ya magaidi'
(last modified Thu, 23 Jan 2025 07:49:11 GMT )
Jan 23, 2025 07:49 UTC
  • Trump akosolewa kwa kuirejesha Ansarullah katika 'orodha ya magaidi'

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekosoa vikali hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kuanzisha mchakato wa kuirejesha Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha ya Washington ya makundi ya 'kigaidi'.

Jana Jumatano, Trump alitia saini amri ya kiutendaji inayomuagiza Waziri wa Mambo ya Nje kuwasilisha ripoti "kuhusu kuitambua Ansarullah kama shirika la kigeni la kigaidi."

Vijana katika mitandao ya kijamii wanasema hatua hiyo dhidi ya Ansarullah itafanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi nchini Yemen.

Wengine wanasisitiza kuwa, kuliweka kundi la Ansarullah katika orodha ya makundi ya kigaidi kutaeneza njaa huko Yemen na kufanya kuwa ngumu zaidi shughuli za mashirika ya ufikishaji misaada ya kibidamu nchini humo. 

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, uamuzi huo wa Marekani dhidi ya Ansarullah ya Yemen ni sawa na kutolewa hukumu ya kifo kwa Wayemen wasio na hatia.

Ikumbukwe kuwa, Januari mwaka 2021, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo, Mike Pompeo alitangaza kuiweka Harakati ya Ansarullah katika orodha ya Washington ya makundi ambayo inayataja kuwa ya kigaidi, siku moja tu kabla ya kumalizika muhula wa kwanza wa Trump.

Hata hivyo utawala uliongia madarakani wa Rais Joe Biden uliwaondoa Wahouthi kutoka kwenye orodha hiyo nyeusi mnamo Februari 2021, ukisema kuwa hatua hiyo ingezuia uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu.