Trump: Dola bilioni 600 inazotaka Saudia kuwezeka Marekani hazitoshi
Rais Donald Trump ametoa wito kwa Saudi Arabia kuongeza kiwango cha uwekezaji wake nchini Marekani hadi dola trilioni moja.
Trump alisema hayo katika hotuba yake kwa njia ya video kwenye mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia huko Davos, Uswisi na kufichua kwamba, Riyadh inapanga kuwekeza dola bilioni 600 katika uchumi wa Marekani, lakini amesisitiza kuwa pesa hizo hazitoshi na inapasa kufikia dola trilioni moja.
Trump amesema, "Nitamwomba Mwanamfalme (wa Saudia, Muhammad Bin Salman), ambaye ni mtu mzuri sana, aongeze ifikie dola trilioni moja, nadhani watafanya hivyo kwa sababu tumekuwa wema sana kwao."
Shirika la habari la serikali ya Saudi Arabia SPA liliripoti karibuni kwamba, Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, alimwambia Trump kwamba nchi yake iko tayari kutoa dola bilioni 600 za uwekezaji katika miaka minne ijayo.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, katika muhula wake wa kwanza, Trump alikuwa akiidunisha na kuidhalilisha Saudi Arabia na kusema Wasaudia hawana lolote isipokuwa fedha tu.
Rais huyo wa Marekani ambaye ameanza muhula wake wa pili wa uongozi siku chache zilizopita, aliwafananisha viongozi wa Saudi Arabia na ng'ombe anayekamwa maziwa, akitangaza wazi kwamba ni ulinzi wa Washington ndio unaowaweka madarakani viongozi hao wa Saudia, hivyo lazima walipe gharama za ulinzi huo.