Waislamu waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hijabu
(last modified Sun, 02 Feb 2025 12:27:29 GMT )
Feb 02, 2025 12:27 UTC
  • Waislamu waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hijabu

Waislamu katika maeneo mbalimbali jana waliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hijabu.

Jana tarehe Mosi Februari 2025, ilisadifiana na kuitimia mwaka wa 13 wa "Siku ya Hijabu Duniani", ambayo huadhimishwa barani Ulaya na Marekani na mashirika ya Kiislamu kwa lengo la kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake wa Kiislamu.

Siku ya Hijabu Duniani ni moja ya hafla za kimataifa zinazohusiana na jinsi wanawake wanavyovaa katika jamii. Katika siku hii, wanawake wote, bila kujali dini au rekodi zao za huko nyuma hushajiishwa na kuhamasishwa kuvaa vazi la stara na staha la Kiislamu la Hijabu ili kupata tajiriba na uzoefu wa siku moja ya maisha ya mwanamke Muislamu.

Lengo la kuadhimisha siku hii ni kusahihisha dhana potofu kuhusu hijabu na wanawake wa Kiislamu na kufikisha ujumbe huu kwa wanawake wa dunia kwamba, hijabu hamukwazi na kumzuia mwanamke kufanya shughuli zake za kijamii.

Jumuiya ya Kitaifa ya Elimu ya Marekani imewataka walimu na wanafunzi kushiriki katika sherehe za siku hii kwa kuwaunga mkono wasichana na wanawake wa Kiislamu wanaokabiliwa na ubaguzi kutokana na kuvaa hijabu.

 Siku hii ni sehemu ya juhudi zinazolengwa kupambana na fikra finyu, ubaguzi, na chuki wanayokabiliana nayo wanawake wa Kiislamu kutokana na kuvaa hijabu.

Waandaaji wa maadhimisho haya walisisitiza kuwa siku hii ni fursa ya kuonyesha thamani ya utofauti na kuiadhimisha kuwa ni nguvu inayounganisha dunia.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani, CAIR, ambalo ndilo shirika kubwa zaidi la kutetea haki za Waislamu nchini Marekani, limetangaza kuwa, mwaka huu, Siku ya Hijabu Duniani imeadhimishwa chini ya kauli mbiu “Hijabu, sauti ambayo haitanyamazishwa."