Waislamu wa Marekani; kitovu cha kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12385-waislamu_wa_marekani_kitovu_cha_kinyang'anyiro_cha_uchaguzi_wa_rais
Hotuba ya Khizr Khan, baba wa askari mmoja Mmarekani Muislamu aliyeuawa katika vita vya Iraq, kwa mara nyengine tena imeifanya hali na nafasi ya Waislamu kuwa kitovu cha kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 01, 2016 02:20 UTC
  • Waislamu wa Marekani; kitovu cha kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais

Hotuba ya Khizr Khan, baba wa askari mmoja Mmarekani Muislamu aliyeuawa katika vita vya Iraq, kwa mara nyengine tena imeifanya hali na nafasi ya Waislamu kuwa kitovu cha kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Hillary Clinton, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrats amewataka wananchi wa Marekani kuwa pamoja na familia ya Khan. Donald Trump, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republicans amemwita Khizr Khan kikaragosi cha Wademokrati. Khizr Khan mwenye asili ya Pakistan ambaye mwanawe Humayun aliuawa katika vita vya Iraq alihutubia kongamano la taifa la chama cha Democrats na kutamka kuwa endapo sera za ujenzi wa ukuta za Trump zitatekelezwa, watu kama yeye hawatoweza kwenda Marekani ili watoto wao waweze kuuawa vitani kwa ajili ya nchi hiyo. Hotuba ya Khan ilishangiriwa mno na hadhirina wa kongamano hilo. Kufuatia kauli hiyo, Donald Trump alidai kuwa hotuba iliyotolewa na baba huyo wa afisa wa jeshi la Marekani aliyeuawa katika vita nchini Iraq iliandikwa na Hillary Clinton.

Khizr Khan alipohutubia kongamano la chama cha Democrats

Hotuba ya Mmarekani Muislamu katika kongamano la kitaifa la Wademokrati imeamsha tena hisia za udadisi juu ya hali ya Waislamu nchini Marekani. Kabla ya Septemba 11 mwaka 2001 Waislamu walikuwa zaidi ni watu wa pembeni katika matukio ya kisiasa na kijamii ya Marekani; na mtazamo wa viongozi wa Marekani kwa Uislamu na Waislamu ulikuwa zaidi ukitathminiwa katika kalibu ya sera za nje na za kijeshi za nchi hiyo.

Waislamu wa Marekani wakiandamana kudai haki sawa kama raia wengine wa nchi hiyo

Baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 yaliyolenga miji ya New York na Washington, Wamarekani Waislamu na Waislamu wanaoishi Marekani waliandamwa na dhoruba ya wimbi la hofu na chuki dhidi ya dini yao.

Mashambulio ya Septemba 11, 2001 yalichochea chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Marekani

Ripoti rasmi zinaonyesha kuwa kuanzia wakati huo na kuendelea hujuma za kushambuliwa na kupigwa Waislamu wa Marekani kwa sababu ya imani yao ya kidini ziliongezeka. Bila ya shaka si viongozi na wanasiasa tu wa Marekani waliokuwa wakikoleza kuni za moto wa chuki na hofu juu ya Uislamu bali vyombo vya habari, taasisi za utafiti pamoja na makundi mengi ya wananchi wa kawaida walikuwa wakiwaangalia Waislamu kwa jicho la kuwa ni watu magaidi na wapenda ukatili. Ilhali makundi, harakati pamoja na maulamaa wa madhehebu tofauti za Kiislamu walikuwa wakilaani vikali vitendo vyovyote vya kigaidi na vya kufurutu mpaka.

Hisia za chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani

Kauli hizo za Waislamu hazikuwa zikisikika wakati vyama vikuu vya siasa nchini Marekani vilipokuwa havina haja ya kura za waungaji mkono na wapinzani wa kampeni za kueneza chuki na hofu juu ya Uislamu. Kwa sababu hiyo licha ya serikali ya Barack Obama ya chama cha Democrats kubadilisha lugha kuhusiana na kadhia muhimu za Ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu haikuchukua hatua zozote za maana kukubaliana na uenezaji sumu ya chuki dhidi ya Uislamu ndani ya Marekani kwenyewe. Hillary Clinton, anayegombea urais kwa tiketi ya chama hicho, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 alitekeleza sehemu ya sera za uenezaji chuki dhidi ya Uislamu za serikali ya Washington. Kwa mujibu wa kauli za baadhi ya shakhsia wa Marekani kundi la kigaidi la Daesh ni matunda ya siasa zilizotekelezwa katika kipindi cha uwaziri wa Hillary Clinton.

Hillary Clinton, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrats

Daesh, sasa imekuwa nembo ya kuchafua sura ya Uislamu duniani. Ilikuwa katika kipindi Hillary Clinton alipokuwa Waziri wa mambo ya Nje nchi ya Libya ilipotumbukia kwenye lindi la vita na machafuko; na moto wa vita ulipowashwa nchini Syria. Katika kila moja kati ya vita na machafuko hayo roho za maelfu ya Waislamu wasio na hatia zilipotea.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh

Bila ya shaka Wademokrati na Hillary Clinton mwenyewe ameamua kuipigia upatu ajenda ya kutetea haki za Waislamu  katika kampeni zake za uchaguzi ili kuvunja nguvu ya uungaji mkono wa Wamarekani wanaotetea ubaguzi wa rangi wa Donald Trump.

Donald Trump, mgombea urais kwa tiketi ya Republicans

Sera za Wademokrati  kuhusiana na haki za Wamarekani Waislamu na Waislamu wa maeneo mengine ya dunia ni za kistaarabu zaidi kulinganisha na mitazamo ya chuki na ubaguzi wa waziwazi wa Trump na waungaji mkono wake. Pamoja na hayo, tajiriba imeonyesha kuwa utendaji wa viongozi wa Marekani kutoka vyama vyote viwili vikubwa vya siasa vya nchi hiyo kuhusu na Uislamu hauna tofauti ya hivyo. Imeshashuhudiwa mara kadha wa kadha wagombea katika uchaguzi nchini Marekani wakisahau ahadi walizotoa mara baada ya kupata ushindi. Ndio kusema kuwa hakuna uhakika kwamba mara baada ya uchaguzi wa mwezi Novemba, viongozi wa chama cha Democrats wataendeleza msimamo wa kukabiliana na sera za Waripablikani za chuki dhidi ya Uislamu.../