Amnesty International: Netanyahu anapaswa kukamatwa na kupelekwa The Hague
(last modified Wed, 02 Apr 2025 03:06:29 GMT )
Apr 02, 2025 03:06 UTC
  • Amnesty International: Netanyahu anapaswa kukamatwa na kupelekwa The Hague

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, mwaliko wa Hungary kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuzuru nchi hiyo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, na Budapest inapaswa kumkamata na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Amnesty International imeongeza kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mbali na kuwalenga raia kwa makusudi na kufanya jinai dhidi ya binadamu, pia anafanya jinai za kivita na kutumia njaa kama silaha ya vita katika Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeonya kuwa safari yoyote ya Netanyahu katika nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) bila ya kukamatwa itauhamasisha utawala wa Israel kuendelea kufanya jinai.

Taarifa hiyo ya Amnesty International imetolewa baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel kutangaza kuwa Netanyahu amepanga kuelekea Hungary leo Jumatano kwa ziara rasmi ya siku nne.

Hungary ni miongoni mwa washirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Ulaya na shirika la NATO.

Itakumbukwa kuwa, Oktoba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko The Hague ilitoa hati ya kukamatwa Netanyahu na Gallant kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kutumia njaa kama silaha dhidfi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.