China yajibu mapigo; yaongeza ushuru wa 84% kwa bidhaa za US
China imesisitiza kuwa "itapambana hadi mwisho" mkabala wa vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Katika hali ambayo ushuru wa juu wa Washington wa asilimia 104 kwa bidhaa za China zilianza kutekelezwa jana Jumatano, Beijing imejibu mapigo na kusema ushuru kwa bidhaa za Marekani utapanda hadi 84% kutoka 34% iliyotangaza hapo awali, kuanzia leo Aprili 10.
Serikali ya Beijing imeeleza bayana kuwa, ikiwa Marekani "itashupalia kuongeza vikwazo vyake vya kiuchumi na kibiashara, China ina nia thabiti na njia nyingi za kuchukua hatua zinazofaa, na itapambana hadi mwisho."
Katika taarifa tofauti, Wizara ya Biashara ya China iliionya Washington jana Jumatano kwamba, "hakuna washindi katika vita vya biashara."
"China haitaki (vita), lakini serikali haitaruhusu kamwe haki halali na maslahi ya watu wa China kudhuriwa au kutwaliwa," imeeleza taarifa hiyo.
Wizara ya Biashara ya China imeongeza kuwa: Trump anatumia ushuru "kama chombo cha kutoa mashinikizo ya juu zaidi kwa ajili ya maslahi binafsi; huu ni uchukuaji wa wazi wa hatua za upande mmoja, ubabe na uonevu wa kiuchumi.