Kauli mbali mbali baada ya kifo cha Papa Francis
(last modified Fri, 25 Apr 2025 02:44:48 GMT )
Apr 25, 2025 02:44 UTC
  • Kauli mbali mbali baada ya kifo cha Papa Francis

Kufuatia kifo cha Papa Francis, baada ya miaka kumi na miwili usukani, macho ya vyombo vya habari na duru za kisiasa yameelekezwa tena kwa makao makuu ya Kanisa Katoliji, Vatican.

Baada ya taarifa za kifo cha Papa Francis mwenye umri wa miaka 88, salamu za rambirambi kutoka pande mbalimbali zimeendelea kumiminika Vatican.

Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alituma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Papa Francis. Katika ujumbe huo, Pezeshkian alisema: "Papa Francis, akiwa kiongozi wa Wakatoliki, alitumia maisha yake ya thamani kueneza mafundisho ya Isa Masih (AS)-yaaniYesu Kristo- hasa kuhusu amani, haki, uhuru, mazungumzo baina ya dini na juhudi za kufanikisha amani, urafiki na usalama wa dunia. Jitihada zake zilikuwa na athari kubwa na zitabaki kuwa kumbukumbu ya kudumu."

Rais wa Iran pia alisifu misimamo ya kibinadamu ya Papa Francis, akibainisha kuwa: "Miongoni mwa mambo ya kipekee ya maisha na uongozi wake ni msimamo wake wa wazi na wa kijasiri dhidi ya vitendo visivyo vya kibinadamu duniani, hasa kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel huko Gaza, na wito wake wa kusitisha mauaji ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Kipalestina. Msimamo huu utabaki katika nyoyo za watu wote waadilifu na wenye hamu ya haki duniani."

Wazayuni wameonyesha hasira kali kutokana na misimamo ya Papa Francis dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na uungaji mkono wake kwa watu wa Gaza. Msimamo huu wa Papa ulisambaratisha propaganda na udanganyifu wa Kizayuni kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Gaza. Baada ya tangazo la kifo cha Papa, gazeti la Maariv lililochapishwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) lilimnukuu Dror Eydar, balozi wa zamani wa utawala wa Kizayuni nchini Italia, akisema: "Israeli haipaswi kushiriki katika mazishi ya Papa Francis, kiongozi wa Wakatoliki duniani, kwa sababu alikuwa mtu mwenye chuki dhidi ya Wayahudi."

Eydar aliendelea kudai kuwa: "Ikiwa tunathamini heshima yetu, basi 'Israel' haipaswi kushiriki katika mazishi hayo."

Sio tu Papa, bali pia mitazamo ya watu wa Magharibi wamezinduka na kufahamu asili ya kibaguzi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Maandamano na mikusanyiko mikubwa ya kupinga Israel na kuunga mkono watu wa Palestina imefanyika katika miji ya Ulaya na Marekani, ikiashiria hali halisi ya kimataifa.

Papa Francis alijulikana kwa unyenyekevu wake, maisha ya kawaida, kupunguza taratibu za kifahari, kusisitiza haki ya kijamii na kuonyesha mapenzi kwa maskini.

Alikuwa na mtazamo wa ukosoaji dhidi ya ubepari wa kupindukia na tamaa ya kupita kiasi ya madola ya Magharibi. Aidha tofauti na mapapa waliomtangulia, aliishi katika makazi ya kawaida ndani ya Vatican badala ya kasri ya kipapa. Alipunguza matumizi ya zawadi kutoka kwa Vatican na kupunguza mishahara ya makadinali. Mojawapo ya sifa za kipekee za Papa Francis ilikuwa ni juhudi zake za kukuza mazungumzo ya kidini. Mahusiano na viongozi wa dini mbalimbali yaliimarika wakati wake, hasa katika vyuo vya dini vya Qom nchini Iran,  Najaf nchini Iraq na Al Azhar nchini Misri.

Papa Francis alishiriki mikutano ya mara kwa mara baina ya wanazuoni wa Kiislamu na viongozi wa Kikristo, Wayahudi wa Iran na wa mataifa mengine. Daima alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mahusiano ya dini kwa dini.

Papa Francis akiwa na Ayatullah Sistani

Pengine tukio muhimu zaidi la mazungumzo kati ya Uislamu (hasa Ushia) na Ukristo katika karne za hivi karibuni lilikuwa ni mkutano wa Papa Francis na Marjaa wa Kishia huko Najaf. Mkutano huo ulifanyika mwaka 2020, wakati Papa Francis alipotembelea Iraq na kukutana na Ayatullah Sistani nyumbani kwake. Katika mkutano huo, Ayatullah Sistani alizungumzia mateso yanayokumba mataifa mbalimbali duniani, akigusia dhulma, umaskini, na ukosefu wa haki za kijamii, pamoja na vita, vikwazo, na kuwafurusha watu, hasa dhidi ya Wapalestina. Alisisitiza wajibu wa viongozi wa kidini na wa kiroho katika kukomesha mateso hayo.

Papa Francis naye alisisitiza umuhimu wa urafiki na ushirikiano baina ya dini, akimshukuru Ayatullah Sistani kwa uungaji mkono na utetezi wake kwa watu wa Iraq dhidi ya vurugu na mateso. Aliomba dua kwa ajili ya amani na undugu katika Iraq, Asia Magharibi, na ulimwenguni kote.

Papa alikuwa kiongozi wa kidini wa Wakatoliki zaidi ya bilioni 1.3 duniani. Hivyo, kifo chake kimepokelewa kwa huzuni  katika maeneo mbali mbali ya dunia. Papa Francis, ambaye jina lake la kuzaliwa lilikuwa Jorge Mario Bergoglio, alichaguliwa kuwa Papa mwaka 2013. Alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na wa kwanza kutoka kwa kundi la Kikatoliki la Kijesuiti. Katika kipindi chake cha upapa, alijulikana kama kiongozi mwenye maono ya mabadiliko na aliyekuwa na juhudi kubwa za kuleta mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki.

Papa Francis alichaguliwa katika kipindi ambacho Vatican ilikuwa ikikabiliwa na migogoro ya maadili katika nchi nyingi. Kwa mwenendo na maneno yake, alijitahidi kujiweka karibu na watu—hasa maskini na walio wachache—na kuziba pengo kati ya Kanisa na wafuasi wake. Jarida la Time lilimtaja kama "Papa wa watu", ambaye kila mara alijitahidi kusogea karibu na jamii na kupunguza tofauti kati ya Kanisa na jamii.