Katibu Mkuu wa UN: Akili Mnemba ni upanga wenye makali pande mbili, ina manufaa na madhara
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, waandishi wa habari wanakabiliwa na hatari kila uchao na kwamba teknolojia mpya ya akili mnemba au AI inayotumika katika tasnia hiyo licha ya kuwa na manufaa inaibua hatari mpya pia kwenye uhuru wa kujieleza.
Guterres ameyasema hayo katika ujumbe aliotoa kwa mnasaba wa siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari inayoadhimishwa leo Mei 3 na kusisitiza kuwa, uhuru wa vyombo vya habari si anasa bali ni hitajio muhimu kwa ajili ya haki, uwajibikaji, na ulinzi wa haki za binadamu.
“Uhuru wa watu unategemea uhuru wa vyombo vya habari. Uandishi huru na wa kujitegemea ni huduma ya msingi kwa umma. Waandishi wa habari wanaposhindwa kufanya kazi yao, sisi sote tunapoteza,” ameeleza Katibu Mkuu wa UN katika ujumbe wake huo.
Akifafanua hatari wanazokumbana nazo waandishi wa habari, Guterres amesema, pamoja na kudhibitiwa kwenye kazi zao, wanakumbwa pia na vitisho, ukatili, na hata kuuawa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza: “masikitiko yangu makubwa ni kwa ongezeko la mauaji ya waandishi wa habari, hasa katika maeneo yenye migogoro kama Ghaza”.
Akigeukia maudhui ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu yanayomulika matumizi ya akili mnemba kwenye uandishi wa habari, Guterres amefananisha akili mnemba na upanga wenye makali pande mbili.
“Ingawa akili mnemba au AI inaweza kusaidia kukuza uhuru wa kujieleza, teknolojia hiyo hiyo pia inaweza kusambaza habari potofu, kuchochea ubaguzi, na kuendeleza hotuba za chuki,” amesema Katibu Mkuu wa UN.
Kwa mujibu wa Guterres, mchakato wa upendeleo wa kukublika kwa taarifa, uongo wa wazi, na hotuba za chuki ni kama mabomu yaliyofichwa kwenye njia kuu za kusambaza taarifa.
Ameongezea kwa kusema: “habari sahihi, thabiti, na zinazotegemea ukweli ni silaha bora ya kuzuia taarifa hizo za uongo”.../