Umoja wa Ulaya na juhudi za kupata washirika wapya wa kibiashara
Vitendo vya Rais Donald Trump wa Marekani hususan kuanza kwa vita vya kibiashara na dunia ambavyo vimesababisha machafuko katika mfumo wa uchumi na biashara wa kimataifa, vimeufanya Umoja wa Ulaya kutaka kupanua na kuimarisha uhusiano wake na nchi za Bahari ya Pasifiki (Trans-Pacific).
Maafisa wakuu wa Ulaya na wanadiplomasia wanaona kurejea kwa Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House kuwa ni kichocheo cha kufufua mpango uliokwama wa kuunda ushirikiano wa kimkakati kati ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kibiashara ya Pacific.
Haya yanajiri baada ya Trump kutangaza ushuru Aprili 2, unaojulikana kama "Siku ya Uhuru," na mipango ya kujenga uhusiano na ushirikiano imara kati ya Brussels na jumuiya ya kibiashara, inayojumuisha nchi 12 zikiwemo Canada, Japan na Mexico, unaosukumwa kwa kasi zaidi kuliko hapo awali.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema pande zote mbili zilitaka kufanya kazi pamoja kwa sheria ili kuhakikisha mazoea ya biashara ya haki duniani kote kwa manufaa ya binadamu. Alisisitiza kuwa kambi zote mbili zilikuwa zikichunguza ni mambo gani yanahitajika kuboreshwa katika WTO katika msukosuko wa sasa na jinsi gani wanaweza kufanya kazi kwa karibu zaidi kufanikisha hili.
Majaribio ya hapo awali ya kuimarisha uhusiano kati ya kambi hizo mbili mnamo 2023 hayakupokelewa vyema. Lakini ripoti ya Bodi ya Kitaifa ya Biashara ya Uswidi inapendekeza kwamba makubaliano kati ya kambi hizo yanaweza kuzifanya kuwa "kitovu cha mvuto wa biashara ya kimataifa."
Mkataba wa Kina na wa Maendeleo wa Ushirikiano wa Pasifiki (CPTPP) ulianzishwa mwaka wa 2018. Mkataba huu ni mkataba wa kibiashara kati ya nchi kadhaa za Ukanda wa bahari ya Pasifiki ambao unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kupunguza ushuru na kuunda sheria za kawaida katika maeneo kama vile uwekezaji na biashara ya kidijitali na unajumuisha mataifa ya Australia, Brunei, Kanada, Chile, Japan, Malaysia, Mexico, New Zealand, Peru, Singapore, Uingereza na Vietnam. Nchi nyingine zinazotaka kujiunga na mkataba huu ni pamoja na Uchina, Taiwan, Ukraine, Costa Rica, Uruguay na Ecuador.

Umoja wa Ulaya kwa sasa una makubaliano baina ya nchi hizo. Wizara ya mambo ya nje ya Kanada pia ilisema nchi hiyo imejitolea kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na Ulaya na eneo la Indo-Pacific. Mawaziri wakuu wa New Zealand na Singapore pia wameidhinisha wazo la kuimarisha ushirikiano kati ya kambi hizo mbili katika wiki za hivi karibuni.
Wanadiplomasia wa Ulaya wameeleza kuwa baada ya kuundwa kwa serikali mpya nchini Australia, mazungumzo ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Canberra yanatarajiwa kuanza tena.
Mnamo Aprili 2, 2025, Donald Trump alitangaza, katika hatua isiyokuwa ya kawaida na yenye utata, kutoza ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi na maeneo 185. Ushuru usiobadilika wa 10% ulianza kutumika tarehe 5 Aprili, na ushuru tofauti ulianza kutumika Aprili 9. Trump pia alizindua ushuru wa 10% kwa bidhaa za Uingereza na ushuru wa 20% kwa bidhaa za Umoja wa Ulaya.
Sambamba na hatua hiyo, Trump aliongeza ushuru kwa bidhaa kutoka China hadi 145%. Kwa kujibu hatua hiyo ya Trump, Beijing iliweka ushuru wa 125% kwa uagizaji wa bidhaa za Marekani. Bila shaka, kutokana na matokeo mabaya ya sera yake mpya ya ushuru, Trump alilazimika kutangaza kusitisha kwa siku 90 utekelezaji wa ushuru mpya, isipokuwa kwa China.
Kufuatia tangazo la Trump la ushuru mpya, masoko ya fedha ya kimataifa yalianza kuwa na utendaji mbaya, huku faharasa nyingi za hisa na thamani za sarafu za Asia na Ulaya zikishuka. Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wameonya kuwa hatua hii inaweza kuleta kipindi cha mdororo wa uchumi duniani na kupanda kwa mfumuko wa bei.

Trump amechukua mbinu ya vitisho, mashinikizo na ubabe kuwalazimisha washirika wa kibiashara wa Marekani kukubali na kutii matakwa ya Washington. Hii itamaanisha vita vya kila upande vya kibiashara na mataifa mengi yanayoinukia kiuchumi, hasa Uchina, pamoja na Umoja wa Ulaya, hasa Ujerumani kama nchi muhimu zaidi katika umoja huo, pamoja na washirika wa kambi za Magharibi kama vile Kanada, Mexico, Japan na Korea Kusini.
Weledi wa mambo wanaonya kuwa, kushadidi vita vya kibiashara na sisitizo la Trump la kutoza ushuru mpya kutakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa dunia. Wakati huo huo, hata washirika wa kistratejia wa Marekani, kama vile Uingereza, hawajaepushwa na athari za ushuru mpya wa Trump, na kwa sababu hiyo, licha ya hamu yake ya hapo awali ya kujiondoa Umoja wa Ulaya kadiri inavyowezekana, London sasa imechukua mtazamo tofauti.
Sasa, kutokana na azma ya Umoja wa Ulaya ya kutafuta washirika wapya wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na eneo la Pasifiki, inaweza kutabiriwa kuwa mataifa mengine makubwa ya kiuchumi duniani, hasa China, yatafuata njia sawa na kutafuta washirika wapya wa kiuchumi na kibiashara zaidi ya Marekani.