Je, vyuo vikuu vya Marekani vimekuwa wenzo wa kisiasa wa serikali ya Trump?
Habari ya kusimamishwa wanachuo zaidi ya 65 wa Chuo Kikuu cha Columbia kwa sababu eti ya kushiriki kwao katika maandamano ya kuiunga mkono Palestina, kwa mara nyingine imefichua makutano nyeti kati ya uhuru wa kujieleza, mamlaka ya kitaaluma na sera za usalama katika vyuo vikuu vya Magharibi.
Uamuzi huu si tu ni radiamali au jibu maalumu bali ni hatua inayoakisi mashinikizo makubwa ya kisiasa na kijamii ambayo yanashuhudiwa katika anga ya taaluma nchini Marekani.
Chuo Kikuu cha Columbia katika hatua yake ya karibuni kimesimamisha kwa muda masomo ya wanachuo zaidi ya 65 walioandamana kuiunga mkono Palestina, na 33 kati yao wamezuiwa kuingia chuoni hapo. Polisi wa Marekani pia wamewakamata wanafunzi 80 walioandamana.

Idadi hiyo kubwa na wanachuo wamenyimwa masomo na kutiwa nguvuni baada ya kuandamana katika Maktaba ya Butler kwa minajili ya kupinga sera za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. New York Post imesema katika ripoti yake kuwa, viongozi wa Chuo Kikuu cha Columbia wametangaza kuwa uamuzi huo umechukuliwa katika kujibu mashinikizo kutoka nje ili kuchukuliwa hatua kali dhidi ya waandamanaji. Mashinikizo haya kwa kiasi kikubwa yanatoka kwa makundi yanayoihami Israel, taasisi za serikali na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinakituhumu chuo hicho kikuu kuwa kinauwanga mkono wanachuo wanaoandamana.
Huku utawala wa Israel ukiendelea kuwaua Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kuzuia misaada kuwafikia wakazi wa Gaza, harakati za maandamano ya wanafunzi zimeongezeka katika vyuo vikuu mbalimbali vya Marekani; ambapo katika miezi michache iliyopita, matukio yasiyopungua matatu kama hayo yametokea katika vyuo vikuu hivyo na kuchochea pakubwa anga ya umma. Kuhusiana na hilo, Aprili 26, mwaka huu wakati wa maandamano ya wanafunzi nchini Marekani, zaidi ya watu 40 walitiwa nguvuni katika Kituo cha Elimu ya Juu cha Auraria huko Denver, Colorado. Katika Chuo Kikuu cha UCLA, mnamo Aprili 17 mwaka huu wakuu wa chuo hicho waliagiza kuondolewa mahema ya wanafunzi waliokuwa wamegoma kwa ajili ya kuonyesha mshikamano wao na Palestina na polisi ya Los Angeles ikawatia nguvu wanachuo zaidi ya 50. Aidha katika Chuo Kikuu cha Michigan, Bodi ya Wadhamini ya chuo hicho hivi karibuni iliamua kusitisha ufadhili wowote wa kifedha wa moja kwa moja kutoka taasisi zinazoendesha shughuli zake katika maeneo yenye migogoro; hatua ambayo imekosolewa na wanaharakati wanachuo.

Uungaji mkono wa wanachuo wa Marekani kwa wananchi wa Palestina na hatua yao ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni umekabiliwa na radiamali ya serikali ya Marekani; kiasi kwamba rais wa nchi hiyo Donald Trump siku kadhaa zilizopita aliwatishia viongozi wa baadhi ya vyuo vikuu vya Marekani kwamba atawakatia bajeti; na baada ya muda mfupi Trump akakata bajeti ya vyuo vikuu vitatu muhimu vya Marekani. Hatua hiyo ilipelekea wakuu wa vyuo vikuu, vyuo na taasisi zaidi ya 100 za elimu nchini Marekani kutoa tamko la pamoja la kupinga hatua ya serikali ya Trump kwa taasisi hizo za elimu ya juu nchini humo. Taarifa hiyo ilikosoa vikali kile ilichokiita "uchokozi usio na kifani wa serikali na uingiliaji wa kisiasa ambao umehatarisha elimu ya juu nchini Marekani.
Pamoja na hayo, mazingira ya kitaaluma katika vvyuo vikuu nchini Marekani yameendelea kuwa chini ya uangalizi mkali, na hatua yoyote ya wanachuo kuandamana inakabiliwa na jibu kali. Aidha hatua yoyote ya kuruhusu maandamano ya kupinga sera za utawala wa Israel inatafsiriwa kuwa sawa na kushirikiana na harakati zilizo dhidi ya Israel. Hii ni katika hali ambayo vyuo vikuu vya Marekani kikiwemo Chuo Kikuu cha Columbia daima vimekuwa vikijiarifisha kama waungaji mkono na washika bendera ya uhuru wa kujieleza na mijadala huru. Kauli mbiu na nara kama "Uhuru wa Taaluma na Kulindwa Maoni Tofauti" kwa miaka kadhaa sasa zimekuwa zikionekana katika milango ya vituo hivyo vya elimu, hata hivyo kusimamishwa na kufukuzwa wanachuo wanaoihami Palestina kunaonyesha kuwa mipaka ya uhuru unaodaiwa kuwepo inabadilika mkabala wa maslahi ya kijiografia na mashinikizo ya kisiasa. Ni wazi kuwa hali hii ya mambo imewapelekea wakuu na marais wa vyuo vikuu vya Marekani kusalimu amri mbele ya sera za Trump, licha ya kauli mbiu zao zote, na si tu kuweka mipaka mkabala wa uhuru wa wanachuo, bali sasa kufukuzwa, kusimamishwa masomo na kukamatwa limekuwa jambo la kawaida katika vyuo vikuu vya Marekani.