Wanafunzi Marekani waanzisha mgomo wa kula kulalamikia njaa iliyosababishwa na Israel huko Gaza
Makundi ya wanafunzi nchini Marekani wameanzisha mgomo wa pamoja wa kususa kula katika kuonyesha mshikamano wao na raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza ambao wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula kutokana na sera za mauaji ya kimbari za Israel.
Harakati hiyo inayoongozwa na wanafunzi wa Marekani pia imekusudia kutoa mashinikizo kwa serikali ya Trump ambayo inawalenga wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaotetea haki za binadamu.
Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Yale na Vyuo Vikuu vinne vya California vimeungana katika harakati hiyo ya kugoma kula.
Wanafunzi hao pia wametaka kutengwa kabisa makampuni yaliyoshiriki katika mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel, kukatwa uhusiano wa vyuo vikuu na taasisi za Israel, na kulindwa uhuru wa kujieleza vyuoni.
Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Marekani waliogoma kula katika kuonyesha mshikamano wao na wananchi wa Palestina wamesema kuwa watakunywa maji tu hadi hapo matakwa yao yatakapotimizwa.
"Watoto na familia kwa ujumla zinashinda njaa kwa kukosa chakula, tumeamua kushikamana na Gaza kwa kuanzisha mgomo wa kula kama aina ya maandamano ya amani ambayo haikiuki sera ya Vyuo Vikuu."
Wanafunzi wa matabaka mbalimbali katika Vyuo Vikuu vya Marekani wameonyesha mshikamano na kuwaunga mkono pakubwa watu wa Gaza dhidi ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni, na wakati huo huo kupinga vikali sera za serikali ya Washington za kuuhami kwa pande zote utawala haramu wa Israel.