Akthari ya Waingereza wanataka Israel iwekewe vikwazo
(last modified Thu, 05 Jun 2025 03:10:33 GMT )
Jun 05, 2025 03:10 UTC
  • Akthari ya Waingereza wanataka Israel iwekewe vikwazo

Utafiti mpya wa maoni uliosimamiwa na Kampeni ya Mshikamano na Palestina (PSC) unaonyesha kuwa, aghalabu ya wananchi wa Uingereza wanaunga mkono kuwekwa vikwazo kamili vya kijeshi dhidi ya utawala wa Israel.

Utafiti huo wa maoni uliofanywa na Shirika la Utafiti la Opinium kati ya tarehe 30 Mei na tarehe 2 Juni, umefichua kuwa asilimia 57 ya Waingereza wanadhani taifa lao linapaswa kuuwekea vikwazo kamili vya silaha utawala wa Israel.

Utafiti huo ulionyesha kuwa, ni asilimia 13 tu ya wananchi wa Uingereza ambao hawaungi mkono hatua hiyo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha utafiti huo umebainisha kuwa, asilimia 53 ya wananchi wa Uingereza wanaitakidi kuwa utawala wa Israel unapaswa kufukuzwa katika Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni, nusu ya watu nchini Uingereza wanaamini kuwa bidhaa zinazotengenezwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) ni lazima zisusiwe.

Kadhalika asilimia 54 ya waliohojiwa wanaunga mkono vikwazo dhidi ya waziri wa fedha wa mrengo mkali wa kulia wa Israel, Bezalel Smotrich, ambaye anaongoza kampeni ya Israel ya kuiweka Gaza chini ya mzingiro kamili; vizingiti ambavyo vimesababisha asilimia 93 ya wakazi wa Gaza kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Jinai za utawala wa Kizayuni ni kubwa mno na hazivumiliki kiasi kwamba hata viongozi wa Uingereza, Canada na Ufaransa wametishia kuiwekea vikwazo Israel kutokana na uhalifu wa kivita na jinai za kutisha huko Ghaza. Tishio hilo limezidisha mashinikizo kwa nduli wa Ghaza, yaani waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.