Lavrov: Makubaliano kuhusu Ukraine lazima yadhamini usalama wa Russia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, suluhisho lolote la mgogoro wa Ukraine lazima liondoe kikamilifu wasiwasi wa kiusalama wa nchi yake.
Lavrov ameyasema hayo mjini Moscow katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud.
Matakwa makuu ya Russia yanajumuisha kupatiwa hakikisho la Ukraine kutojiunga na shirika la kijeshi la NATO, kutokuwa na nguvu za kijeshi, kutambuliwa kimataifa mabadiliko ya maeneo yaliyotekwa vitani na kupatiwa kinga na ulinzi jamii ya Waukraine wanaozungumza Kirusi.
“Hatuwezi kuridhika na suluhisho linaloshindwa kushughulikia maslahi halali kisheria ya usalama wa Russia au kuondoa na kuzuia ukiukaji wa siku za usoni wa haki za Warusi na za jamii zinazozungumza Kirusi” ameeleza Lavrov.
Kwa muda mrefu, Moscow imekuwa ikiitazama hatua ya NATO kujipanua kuelekea mashariki kama tishio kubwa kwa usalama wake wa taifa na kuichukulia hamu ya Ukraine kujiunga na shirika hilo la kijeshi linaloongozwa na Marekani kama kichocheo kikuu cha mzozo wa kijeshi unaoendelea hivi sasa.
Wiki iliyopita, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema, wasiwasi wa nchi yake kuhusu harakati za NATO umekuwa ukiendelea kupuuzwa na kunyamaziwa kimya…/