Mwandishi habari ajiuzulu Reuters akilalamikia hatua ya shirika hilo kuhalalisha mauaji ya Israel dhidi ya waandishi habari
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130024-mwandishi_habari_ajiuzulu_reuters_akilalamikia_hatua_ya_shirika_hilo_kuhalalisha_mauaji_ya_israel_dhidi_ya_waandishi_habari
Mpiga picha wa Canada, Valerie Zink, ametangaza kujiuzulu kutoka kwenye shirika la habari la Reuters, akipinga nafasi ya shirika hilo katika kuendeleza propaganda za Israel na kuhalalisha mauaji ya waandishi wa habari wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Aug 26, 2025 15:14 UTC
  • Mwandishi habari ajiuzulu Reuters akilalamikia hatua ya shirika hilo kuhalalisha mauaji ya Israel dhidi ya waandishi habari

Mpiga picha wa Canada, Valerie Zink, ametangaza kujiuzulu kutoka kwenye shirika la habari la Reuters, akipinga nafasi ya shirika hilo katika kuendeleza propaganda za Israel na kuhalalisha mauaji ya waandishi wa habari wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Zink ambaye alifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea wa Reuters kwa kipindi cha miaka minane, amesema: "Haiwezekani kwangu kudumisha uhusiano na Reuters kutokana na nafasi yake ya kuhalalisha na kuwezesha mauaji ya kimfumo ya waandishi wa habari 245 huko Gaza."  Ameongeza kuwa: "kukariri uongo wa Israel" katika vyombo vya habari vya Magharibi na kutotekeleza kwao majukumu yao ya msingi kama taasisi za uandishi wa habari, vimewezesha mauaji ya waandishi wa habari zaidi katika miaka miwili kuliko idadi ya waliouawa katika Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, vita vya Korea, Vietnam, Afghanistan, Yugoslavia, na Ukraine kwa pamoja."

Mwandishi huyo wa habari wa Canada ameeleza kuwa shirika la habari la Reuters lilichagua kuchapisha madai ya Israel kwamba mwandishi wa Al Jazeera huko Gaza, Anas al-Sharif, aliyeuawa na jeshi la Israel, alikuwa wakala wa Hamas, akisisitiza kwamba huo ulikuwa "uongo mmoja kati ya mwingi ambao vyombo vya habari kama Reuters vimeukariri kibubusa."

Valerie Zink amesema: "Tabia ya Reuters kuendeleza propaganda za Israel haikuokoa maisha ya mwandishi wake kutokana na mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel," akibainisha kuwa waandishi wa habari watano wa Palestina, ikiwa ni pamoja na mpiga picha wa Reuters, Hossam al-Masri, waliuawa katika mashambulizi mawili ya moja kwa moja kwenye Nasser Medical Complex siku ya Jumatatu wiki hii.

Mpiga picha huyo amevishutumu vyombo vya habari vya Magharibi kuwa vinatayarisha mazingira yanayofaa kwa Israel kufanya uhalifu, akinukuu taarifa ya mwandishi wa habari wa Marekani, Jeremy Scahill aliyesema kwamba "kila chombo kikuu cha habari, kama New York Times, Washington Post, Associated Press na Reuters, kinafanya kazi kama wenzo wa kueneza propaganda za Israel, kutakasa jinai za kivita, na kuwavua sifa ya binadamu wahanga wa uhalifu wa Israel.."