Seneta Cruz ataka US ama iitambue Ikhwanul Muslimin kuwa kundi la kigaidi au iwaue wanachama wake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130710-seneta_cruz_ataka_us_ama_iitambue_ikhwanul_muslimin_kuwa_kundi_la_kigaidi_au_iwaue_wanachama_wake
Ted Cruz, Seneta wa Marekani wa jimbo la Texas kwa tiketi ya chama tawala cha Republican amesema, wakati umewadia kwa Marekani kuitambua harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni shirika la kigaidi, kwa sababu hiyo ndiyo hatua mbadala ya kuwaua wanachama na washirika wa harakati hiyo.
(last modified 2025-09-12T06:57:23+00:00 )
Sep 12, 2025 06:57 UTC
  • Seneta Cruz ataka US ama iitambue Ikhwanul Muslimin kuwa kundi la kigaidi au iwaue wanachama wake

Ted Cruz, Seneta wa Marekani wa jimbo la Texas kwa tiketi ya chama tawala cha Republican amesema, wakati umewadia kwa Marekani kuitambua harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni shirika la kigaidi, kwa sababu hiyo ndiyo hatua mbadala ya kuwaua wanachama na washirika wa harakati hiyo.

Cruz ameuambia umati wa watu katika taasisi ya mrengo wa kulia ya Heritage Foundation mjini Washington, DC: "kundi la Ikhwanul Muslimin na matawi yake yanafaa yatambuliwe kama mashirika ya kigaidi kutokana na historia yake ndefu na inayoendelea ya utumiaji nguvu, misimamo mikali na kuvuruga uthabiti". 

Seneta huyo ambaye ni maarufu kwa misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu ameendelea kusema: "hiyo ni sera ya moja kwa moja ya kutumia wakati mtu anakabiliwa na shirika la kigaidi, au kwa uchache suluhisho jingine ni la kuwaua magaidi, ambayo ni sera nzuri sana pia."

Mnamo mwezi Julai, Cruz, ambaye ni mtaalamu wa katiba, alipendekeza Sheria ya mwaka 2025 ya kuitambua Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi, ikiwa ni mara yake ya tano kuwasilisha mswada kama huo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. 

Akibainisha ni kwa nini sasa ni wakati mwafaka wa kuchukua hatua hiyo, seneta huyo amesema: "tuna Bunge la Republican na rais wa Republican ambaye amejitolea kukabiliana na kitisho cha ugaidi wa Kiislamu kwa usalama wa taifa la Marekani. Kwa hiyo tuna machaguo yote mawili ya bunge na serikali".

Aidha, Cruz amesema Washington inahitaji kuungana na washirika wake wa Kiarabu katika suala hilo.

Kwa sasa, harakati kongwe ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin imeorodheshwa kuwa kundi la kigaidi katika Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Syria, Misri na Saudi Arabia. Wakosoaji wa hatua hiyo wamekuwa wakisisitiza kwa muda mrefu kwamba kuitambulisha harakati hiyo ya kisiasa kuwa ni kundi la kigaidi ni hatua inayolenga kuhakikisha haiwi tishio tena kwa watawala wa kifalme na wakiritimba wa madaraka katika nchi za eneo.

Seneta Cruz ameilezea Ikhwanul Muslimin kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani, harakati ambayo ingali ina umaarufuu mkubwa katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kutokana na mitazamo yake ya kuchanganya mafundisho ya asili ya Kiislamu, harakati za kisiasa na programu za ustawi wa jamii.../