Askari 12 wa Pakistan wauawa katika shambulio la kigaidi kaskazini magharibi mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130746-askari_12_wa_pakistan_wauawa_katika_shambulio_la_kigaidi_kaskazini_magharibi_mwa_nchi
Askari wasiopungua 12 wa Pakistan wameuawa katika makabiliano ya kufyatuliana risasi na magaidi kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2025-09-13T07:23:03+00:00 )
Sep 13, 2025 07:23 UTC
  • Askari 12 wa Pakistan wauawa katika shambulio la kigaidi kaskazini magharibi mwa nchi

Askari wasiopungua 12 wa Pakistan wameuawa katika makabiliano ya kufyatuliana risasi na magaidi kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo na kitengo cha habari cha jeshi la Pakistan imesema, mbali na askari hao, magaidi 35 wa kundi lililopigwa marufuku la Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) waliuawa wakati wa operesheni mbili tofauti za kijeshi zilizotekelezwa kuanzia Septemba 10 hadi13.

Katika operesheni ya kwanza iliyotekelezwa na jeshi katika wilaya ya Bajaur, wanamgambo 22 waliuawa, na katika mapigano ya pili yaliyojiri huko Waziristan Kusini, askari 12 na wanamgambo 13 wa kundi la TTP waliuawa pia.

"Makabiliano yote miwili yalihusisha "Fitna al Khawarij," imeeleza taarifa hiyo ya jeshi la Pakistan ikilimaanisha kundi hilo la TTP.

Pakistan imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo katika miaka ya hivi karibuni. Islamabad inaituhumu serikali ya Kabul inayoongozwa na kundi la Taliban kwamba imeshindwa kuwazuia magaidi wa TTP kufanya mashambulizi nchini Pakistan.

Afghanistan kwa upande wake inakanusha tuhuma hizo na kusisitiza kuwa imejifunga kuhakikisha hairuhusu ardhi yake kutumiwa kufanyia mashambulizi dhidi ya nchi jirani.../