UNHCR: Marekani imekuwa ikifukuza wahamiaji kinyume cha sheria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i131728-unhcr_marekani_imekuwa_ikifukuza_wahamiaji_kinyume_cha_sheria
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limekosoa vikali sera za Marekani kuhusiana na wahamiaji na kueleza kwamba, imekuwa ikifukuza wahamiaji kinyume cha sheria.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 07, 2025 23:11 UTC
  • UNHCR: Marekani imekuwa ikifukuza wahamiaji kinyume cha sheria

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limekosoa vikali sera za Marekani kuhusiana na wahamiaji na kueleza kwamba, imekuwa ikifukuza wahamiaji kinyume cha sheria.

Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump imekuwa ikiwafukuza wahamiaji kwa njia zinazokiuka sheria za kimataifa.

Akizungumza mjini Geneva, mkuu huyo wa UNHCR ametumia hotuba yake kulalamikia kupunguzwa kwa ufadhili na rasilimali ndani ya shirika hilo, akibainisha kuwa hatua hiyo imesababisha kupotea kwa takriban ajira 5,000 mwaka huu sawa na karibu robo ya wafanyakazi wake.

Mwezi uliopita Baraza la haki la Umoja wa Afrika (AU) lilielezea wasiwasi wake kuhusu makubaliano ya Washington na nchi kadhaa za Afrika, ambayo yanaruhusu nchi hizo za Kiafrika kupokea wahamiaji waliofukuzwa Marekani.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Afrika inasema, makubaliano hayo yanaweza kukiuka kanuni za msingi, na haki za binadamu na kupewa hifadhi chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na mikataba mingine ya kimataifa na kikanda.

Wakati huo huo, takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zinaonyesha kuwa, karibu watu 9,000 walikufa mwaka jana wakijaribu kuvuka mipaka.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limerekodi vifo vya wahamiaji wasiopungua 8,938 mwaka 2024, na kuweka rekodi mpya kwa mwaka wa tano mfululizo.