China: Marekani inakiuka mamlaka ya kujitawala ya mataifa mengine
Fu cong, balozi na mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amesema kuhusiana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Venezuela kwamba, hatua hiyo ya Washington inakiuka vikali mamlaka ya kujitawala ya mataifa mengine.
Fu Cong amesema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoangazia Venezuela: "Marekani imepeleka vikosi vyake katika bahari ya pwani ya Venezuela katika Karibiani kwa kile kilichoelezwa kuwala kupambana na biashara ya madawa ya kulevya."
Aliongeza kuwa Marekani pia imesababisha "mvutano unaoendelea katika eneo hilo" kwa kukamata boti za Venezuela.
Balozi na mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa hatua za upande mmoja na za kupita kiasi dhidi ya boti za nchi nyingine "zinakiuka haki ya maisha ya wafanyakazi wao na haki nyingine za msingi za binadamu na ni tishio kwa uhuru na usalama wa usafiri wa majini."
Alibainisha kuwa hatua hizi "pia zinakiuka kwa kiasi kikubwa mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine na kutishia usalama na amani ya kikanda."
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ameonya mara kadhaa kuwa shambulio lolote dhidi ya taifa lake litakabiliwa kwa mshikamano wa mataifa ya kanda, akisisitiza kuwa nchi hiyo katu haiwezi kuwa koloni wala kutawaliwa na nguvu za kigeni.
Wiki iliyopita, maelfu ya raia walijitokeza katika mji mkuuu Caracas kuonyesha uungaji mkono wao kwa Rais Maduro na utayari wao kutetea taifa, huku jeshi likionyesha uwezo wake kupitia mazoezi ya kijeshi wakati wa ongezeko la wanajeshi wa Marekani katika Karibiani.