Imam na msaidizi wake wauawa kwa risasi New York, Marekani
Imam wa msikiti mmoja katika jimbo la New York nchini Marekani ameuawa kwa kufyatuliwa risasi katika mazingira ya kutatanisha.
Duru za habari zinaarifu kuwa, Imam Alala Uddin Akongi wa Msikiti wa Jamia wa Al-Furqan na msaidizi wake aliyetambulika kama Thara Uddin waliuawa kwa kufyatuliwa risasi jana Jumamosi walipokuwa wakitoka kuswali swala ya Adhuhuri katika barabara ya Ozone, mji wa Borough of Queens jimboni New York.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani limelaani mauaji hayo na kusema kuwa wawili hao mbali na kuwa viongozi wa kidini, walikuwa viongozi wa kijamii katika mji huo.
Haya yanajiri wiki moja baada ya wanajeshi waliostaafu katika jimbo la Texas nchini Marekani kutishia kuwakata vichwa kwa mapanga Waislamu watakaoenda kutekeleza ibada ya swala katika Msikiti wa Al-Sahaabah mjini Wataunga jimboni hapo. Alia Salem, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani katika eneo la Dallas sambamba na kulaani kitendo hicho, alisema baraza hilo limekuwa likipokea malalamiko kutoka kwa wasimamizi wa msikiti huo ambao wamekuwa wakitishiwa maisha kwa njia ya simu na watu wasiojulikana.
Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka huu, mamia ya Waislamu nchini Marekani waliandamana kupinga hatua za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika mji wa Washington DC huku wakipiga nara kulaani uenezaji wa vitendo vya chuki dhidi yao.